January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM imetaka yote, itakosa yote

Mgogoro wa madiwani Bukoba
Spread the love

BABA wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema wakati wa uhai baada ya mfumo wa vyama vingi kuanzishwa hapa nchini, kuwa uwepo wa vyama vya upinzani hata kama ni vya ovyo ovyo, utakifanya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kabla ya kufanya maamuzi ijiulize kwa makini ili isije ikafanya makosa.

Alilirudia tena hili wakati wa umaarufu wa Augustine Lyatonga Mrema alipojiunga na chama cha NCCR-Mageuzi na kuifanya CCM kuwa na wakati mgumu wa kuamua nani apeperushe bendera yake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.

Mantiki ya Mwalimu ilikuwa ni kuionya CCM kuwa vyama vya upinzani vipo hata kama ni dhaifu. Kwamba, CCM ikifanya makosa katika maamuzi yake, inaweza kupoteza viti katika chaguzi mbalimbali.

Hivi tunashuhudia utekelezwaji wa maonyo ya Mwalimu Nyerere. Tofauti na wakati ule, hivi sasa vyama vya upinzani ni imara zaidi – hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) – kwa upande wa Tanzania Bara na Chama cha Wananchi (CUF) kwa upande wa Zanzibar.

Hali kadhalika, tofauti na wakati ule, hivi sasa CCM kimekuwa dhaifu zaidi. Uimara wa vyama vya upinzani unachangiwa kwa sehemu kubwa na udhaifu wa CCM. Hii ni tofauti na kusema kuwa udhaifu wa CCM umetokana na uimara wa vyama vya upinzani. Hili nimewahi kulijadili katika muktadha wa aina mbili.

Kwanza, umaarufu wa CHADEMA hautokani na uzuri wa sera zake bali unatokana na udhaifu wa CCM. Hii ina maana kilichotangulia ni udhaifu wa CCM, kisha umaarufu wa CHADEMA ukajitokeza.

Pili, tabia ya CCM na makada wake kuikashifu na kuichafua CHADEMA bila kuijenga CCM, ni jambo jingine linalokidhoofisha chama hicho. Kwamba, makada wa CCM wakiongozwa na Mwigulu Nchemba, wanaweza kufanikiwa kuichafua CHADEMA kwa kuiita majina yote mabaya kama chama cha kikabila, kigaidi, kikanda, cha Kikristo, NGO nakadhalika, lakini kwa kufanya hivyo wasiweza kukijenga chama chao. Huku ni sawa na kulaani giza bila kuwasha mshumaa.

Tangu vyama vya upinzani vianze kuimarika na kuruka viunzi vya kununuliwa na kurubuniwa na CCM, udhaifu wa CCM pia umeongezeka sambamba. Udhaifu huo umeonekana katika maamuzi na hatua zinazochukuliwa na chama hicho katika kukabiliana na migogoro ya ndani na nje ya chama hicho.

Udhaifu wa CCM umezidi kuonekana wazi katika mnyukano ulioibuka hivi karibuni katika manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera. Mnyukano ni kati ya madiwani wanane wa chama hicho tawala wakiongozwa na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki kwa upande mmoja, na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk. Anatory Amani kwa upande mwingine.

 Sawa na alivyosema Baba wa Taifa, vikao vya CCM Mkoa na Taifa vimeshindwa kuumaliza kwa muda mrefu kwa sababu kadhaa lakini iliyo kubwa ikiwa ni hofu juu ya CHADEMA.

Tangu mgogoro huo uanze, kumekuwepo na msururu wa viongozi wa kitaifa kwenda Bukoba kusuluhisha huo bila mafanikio. Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula amefika Bukoba. Mwigulu, naibu katibu mkuu (Bara), amefika Bukoba.

Katibu Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amefika mara mbili Bukoba. Katibu Mkuu Abulrahamani Kinana amefika Bukoba. Na hata Mwenyekiti wa Taifa na Rais wa Jamhuri alifika Bukoba na kuliongelea suala hili hadharani. Wote hao walishindwa kulimaliza na kusubiri kulitolea uamuzi ndani ya kikao!

Halmashauri ya CCM Mkoa na vyombo vyake ilijaribu mara kadhaa na hatimaye ikafanya uamuzi mgumu wa kuwafukuza uanachama madiwani wale walio upande wa Kagasheki. Ndani ya masaa 24, CCM Taifa ilibatilisha uamuzi huo. Uamuzi huo uliibua shutuma nyingi zilizovishwa sura za udini, rushwa, ukabila, na uasi dhidi ya itikadi ya CCM.

Katikati ya mnyukano huo, vikao mbalimbali vilikuwa vikisita kufanya maamuzi kwa hofu ya kuwa upande utakaoathirika na maamuzi hayo, utahamia CHADEMA na kushinda uchaguzi mdogo. Hofu hii iligubika uongozi wa CCM ngazi zote na kila aliyejenga hoja ya kutetea upande wowote kati ya pande hizo mbili alihitimisha kwa kusema, “Busara itumike, vinginevyo CHADEMA wataifuta CCM Bukoba.”

Huko nyuma, katika miggoro ya ndani ya CCM yenye sura ya kuasi maamuzi na itikadi kwa chama ilikuwa inaamuliwa haraka pale ambapo hapakuwa na tishio la vyama vya upinzani. Hata sasa, mahali popote ambapo vyama vya upinzani havina nguvu, CCM inafanya maamuzi magumu bila shida yoyote.

Angalia kwa mfano, kikao kilichobatilisha uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kagera, ndicho hicho kilichomfukuza uanachama Mwakilishi wa Kiembesamaki, Unguja, Mansour Himid.

Ilikuwa rahisi kufanya hivyo kwa sababu, CUF haina mizizi mirefu katika jimbo hilo na CCM ina uhakika wa kushinda kiti hicho.

Mazingira haya yanatulazimisha tuamini kuwa uamuzi wa kuwarejesha madiwani wa Bukoba hautokani na Halmashauri Kuu kukosea katiba katika kuwafukuza madiwani wake, bali madiwani hao wameokolewa na uimara wa CHADEMA katika manispaa hiyo.

Lakini kuna hili pia. Sasa zimeibuka tuhuma na shutuma, kwamba CCM Taifa ililazimika kughushi katiba ili kujinasua katika mgogoro wa matumizi ya katiba. Hilo linahitaji nafasi pekee!

Uimara wa CHADEMA uliitisha CCM kwa sababu wakati za ziara ya mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, madiwani waliofukuzwa walionekana wakijadiliana jambo na Mbowe. Uhuru wa madiwani hao waliorejeshwa kuonekana wakinywa soda na viongozi wa CHADEMA ulisababisha mchafuko wa tumbo ghafla katika kambi ya CCM.

Ikumbukwe hoja ya madiwani ya kutaka kumg’oa Meya inaungwa mkono na madiwani wa vyama vya upinzani.

Kwa mara ya kwanza, tumewasikia viongozi wa taifa wa CCM wakitetea uhuru wa madiwani kufanya kazi zao ndani ya halmashuri bila kuingiliwa na itikadi za vyama vyao. Mmoja wao alijenga hoja kuwa, “ikiwa madiwani wa upinzani waliungana na wa CCM wakamchagua Meya ikaonekana ni sawa, inakuwaje haramu tena madiwani hao kuungana na wapinzani kutaka kumng’oa?”

Kinachoonekana wazi sasa mbele ya Watanzania ni jitihada za CCM kutaka kupata vyote kwa wakati mmoja. CCM inataka ibaki na Meya, ibaki na Mbunge, ibaki na madiwani wote, ibaki na udhibiti wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, na ibaki na ufisadi wake inaoupenda sana.

Haijarishi pande mbili hizo zimeumizana kiasi gani, chama kimeumia kiasi gani, wananchi wameumia kiasi gani wakati wa mgogoro huo na serikali ya mkoa imepoteza mwelekeo kiasi gani. Kinachotakiwa ni chama kubaki na wote kwa hofu ya kuwapoteza wakaenda CHADEMA.

 Wahenga wanasema, “Mchelea mwana kulia, hulia yeye” na “Mtaka yote kwa pupa hukosa yote.” Halmashauri Kuu ya Mkoa ilikuwa imeonyesha njia kwa kufanya uamuzi mzuri kwa njia mbaya. Lakini CCM taifa kimeamua kufanya vibaya uamuzi mbaya tena kwa maslahi ya muda mfupi.

Mwisho wa siku, CCM ya sasa inaonekana dhaifu mbele ya umma, inanunulika, inatetemeka mbele ya vyama vya upinzani, na haina inachosimamia isipokuwa kusimamia watu binafsi kwa maslahi binafsi. Chama kinachosimamia kila kitu, huakisimamii chochote. Huishia kuanguka. Huko ndiko chama hiki kinakoelekea.

error: Content is protected !!