August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM, IGP wawakimbia Chadema na Mutungi

Spread the love

KIKAO kilichokuwa kimeitishwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ili kujadili hatima ya kufanyika kwa mikutano ya hadhara hapa nchini kimeota mbawa baada ya baadhi ya wajumbe kushindwa kuhudhuria kikao hicho, anaandika Charles William.

Kikao hicho kilichokuwa kihusishe wajumbe sita akiwemo George Masaju Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Francis Mutungi Msajili wa vyama vya siasa, Abdulrahman Kinana Katibu Mkuu CCM na Dk. Vincent Mashinji Katibu Mkuu CHADEMA.

Wengine waliokuwa wamealikwa kuhudhuria kikao hicho ni Katibu Mkuu wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Ernest Mangu (IGP) Mkuu wa Jeshi la Polisi hapa nchini.

Kikao hicho kilikuwa na ajenda kubwa mbili ikiwemo hatima ya mikutano na maandamano ya vyama vya siasa sambamba na kujadili tamko la CHADEMA kuanzisha operesheni inayojulikana kama UKUTA kuanzia tarehe 01 Septemba, 2016 kote nchini.

Hata hivyo kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe watatu tu ambao ni Bahame Nyanduga, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Dk. Mashinji na Jaji Mutungi huku upande wa Serikali ukiongozwa na Masaju Mwanasheria Mkuu na IGP Mangu pamoja na Kinana, Katibu Mkuu wa CCM wakishindwa kufika.

Wajumbe waliokuwepo walikubaliana kuahirisha kikao hicho mpaka wakati mwingine huku sababu za kutofika kwa baadhi ya wajumbe zikishindwa kuwekwa bayana.

error: Content is protected !!