June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM hakina mvuto tena

Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete akiongoza kikao cha Kamati Kuu.

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinakabiliwa na mtihani mkubwa wa kusambaratika. Wala wanaochangia muanguko wa chama hiki si watu walioko nje ya chama, kwa kweli ni makada wake, wengine wakiwa ndio viongozi wa ngazi ya juu katika serikali anayoiongoza mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete.

Rais Kikwete ambaye aliingia madarakani kwa kampeni kabambe ya kundi la Mtandao likiongozwa na Rostam Aziz na Edward Lowassa, aliheshimika mwanzoni. Yanayotokea sasa, yanaonesha kwamba haheshimiwi kwa uzito ule aliokuwa nao miaka tisa iliyopita.

Utovu wa heshima huo miongoni mwa makada wa CCM na wasaidizi wake, kote katika chama na serikalini, ndio chanzo hasa cha kukihatarisha chama kusambaratika. Mwanzoni iliaonekana kama CCM ingeanguka kwa rushwa tu peke yake.

Sivyo ilivyo leo. Kutoheshimiwa na kutosikilizwa kwa Mwenyekiti Rais Kikwete, kumeongeza uzito wa tatizo kubwa linalokabili chama hicho kilichozaliwa Februari 5, 1977 baada ya kuunganishwa kwa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) cha Tanganyika na Afro-Shirazi Party (ASP) cha Zanzibar.

Mifano mizuri kabisa ya namna Mwenyekiti Rais Kikwete asivyoheshimiwa na kusikilizwa na makada wenzake, ni kushindwa kutekelezwa kwa maagizo yanayotolewa na chama chini ya maelekezo yake.

Mwaka 2012 akiongoza Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Mwenyekiti Kikwete aliridhia maamuzi ya kuwashughulikia makada wanaotajwa sana kwa tuhuma za ufisadi kiasi cha kuwapunguza ari ya kupenda chama wanachama wa kawaida.a

Agizo hilo lililopaswa kusimamiwa na timu ya sekretarieti ya chama ikiongozwa na Katibu Mkuu, Wilson Mukama, wakati huo Makamu Mwenyekiti akiwa Pius Msekwa, halikutelelezwa.

Hakuna kada mtuhumiwa wa ufisadi aliyetii agizo hilo. Rostam, aliyekuwa Mbunge wa Igunga, mkoani Tabora, kwa hiyari yake, bila ya shaka kwa kujisikia anatajwatajwa sana kuwa miongoni mwa watuhumiwa, aliamua kujiuzulu nafasi zote za uongozi.

Mbali na ubunge, pia alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama. Rostam ni mfanyabiashara maarufu nchini aliyeingia katika siasa za waziwazi wakati wa kuelekea uchaguzi mkuua wa 2005. Kwa sehemu kubwa anajulikana kama kinara wa ufadhili wa mkakati wa kumuingiza Ikulu Mwenyekiti Kikwete.

Mfano mwingine ni kinachoendelea kwenye Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma. Vikao vinaendelea pamoja na uamuzi ambao Rais Kikwete aliafikiana na viongozi wenzake wa vyama chini ya mwamvuli wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Rais Kikwete alifanya majadiliano na viongozi wenzake hao mara mbili – Agosti 30 na Septemba 8, siku ambayo walikubaliana kuwa hakuna tena matumaini ya kupatikana kwa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano, na kwa hivyo, ni busara bunge kusitishwa ili kusubiri maandalizi ya marekebisho ya sheria za kuwezesha kufikia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015.

Lakini, badala ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samwel Sitta kuheshimu maafikiano yaliyofikiwa na kiongozi mkuu wa taifa, akiwa ndiye kiongozi wake vilevile, ameshikilia kuendelea kuongoza bunge hilo.

Kila mwenye akili tulivu anajiuliza, hizi jeuri alizonazo Sitta amezipata wapi? Au ndivyo chama atokacho, CCM, kilivyomtuma? Au ni kwa sababu hakuna anayemuogopa? Au shauri ya tamaa tu ya fedha kwa kuwa katika zile Sh. 21 Bilioni zinazotumiwa kwa ajili ya posho ya wajumbea, ana fungu lake la Sh. 150 Milioni hivi?

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema yapo mambo mengi katika yanayotokea. Ila ukweli ulio wazi ni kwamba CCM kimepoteza mvuto na kufikia hatua kuwa kila kada anajifanyia atakavyo.

error: Content is protected !!