September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

CCM = Chama Cha Magufuli?

Spread the love

MWENYEKITI mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Pombe Magufuli, anaweza kujenga utamaduni mpya ndani ya chama chake. Utamaduni wa kujimilikisha chama na maamuzi yake, anaandika Kondo Tutindaga.

Huko nyuma wakati wa uongozi wa Julius Nyerere, walitokea makada wa CCM waliompenda Nyerere hadi kupitiliza.

Yeye kwa nia njema, alikuwa amewapa fursa ya kwenda kujifunza namna ya kuendesha vyama vya ukombozi na kimapinduzi huko Burgaria, Korea, China, Cuba, Urusi na nchi nyingine za kijamaa.

Lengo la Nyerere lilikuwa ni kitafuta njia bora ya kuvifanya vyama vibakie ni vya wanachama na si vya viongozi. Waliporejea nchini wakaanzisha salaam maalum iliyosema “zidumu fikra za mwenyekiti.”

Salaam hiyo ikashika kasi nchi nzima. Baadhi ya makada wazoefu wakairekebisha na kuifanya isomeke “zidumu fikra sahihi za mwenyekiti.”

Baada ya kimya kirefu, Nyerere katika moja ya vikao vya Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) ya chama chake, kwa mshangao wa wengi, akaipiga marufuku salaam hiyo. Baba wa taifa hakupenda kuabudiwa wala kutukuzwa.

Kwa uzoefu wangu wa kumfahamu Baba wa taifa hili, sikuwahi kumsikia hadharani akiomba wananchi wamwombee kwa kazi ngumu na kubwa aliyokuwa anaifanya.

Alipendwa na watu bila kuwaomba wampende na hakutuma watu waende mitaani kukamata watu waliokuwa wanamsema vibaya.

Hata hivyo, walikuwapo watu wa idara ya usalama (kitengo maalum), waliokuwa wakichunguza mbinu za mabeberu wanavyoweza kuingia nchini. Kikosi hiki kiliweza kuwashughulikia baadhi ya watu waliokutwa wakimsema vibaya, lakini hakikuwa kimetumwa na kufanya hivyo.

Hata wakati alipopata fursa ya kukutana na viongozi wa dini ana kwa ana katika faragha, hakuwaomba wamwombee. Badala yake, aliwahimiza kuliombea taifa na Watanzania ili waupende ujamaa.

Licha ya yeye kuwa Mkatoliki anayesoma sala zilizoandikwa, aliomba mara nyingi akiwatanguliza watanzania waupende ujamaa na Azimio la Arusha. Baadhi ya madhehebu yalikuwa yana utaratibu wa kumwombea katika vitabu vya sala na kuandika jina lake kabisa.

Hakupenda hali hiyo, na aliwatuma wasaidizi wake waaminifu kuongea na makanisa hayo kuondoa jina lake katika vitabu vya sala vya madhehebu hayo. Hii inaeleza jinsi Baba wa taifa alivyokuwa mnyenyekevu na nina kila sababu ya kuamini unyenyekevu wake ndilo chimbuko la umaarufu wake.

Baba wa taifa alifanya kazi kubwa kitaifa na kimataifa. Alikuwa na maadui ndani na nje. Kipindi hicho cha vita baridi, Mwalimu alikuwa tishio kwa mataifa makubwa kama Marekani, Uingereza na hata Urusi. Kwa Wamarekani na waingereza alionekana mkomunisti, na kwa Warusi hakuaminika sana maana alionekana kuukataa ukomunisti na kuupenda ujamaa.

Kwenye ukanda wa kusini mwa Afrika, Baba wa Taifa alikuwa na maadui wakubwa (makaburu), waliotafuta kwa udi na uvumba kuitoa roho yake. Pamoja na ukweli huo, hatukumsikia akiwaambia watanzania wamwombee. Tulisikia viongozi wa dini wakihimizana kumwombea Baba wa Taifa kama mkuu wa nchi yenye agenda kubwa na ya hatari ndani na nje ya nchi.

Licha ya Nyerere kuenziwa, kutungiwa nyimbo na mashairi, kutukuzwa ndani na nje ya taifa letu, hatukumsikia hadharani akisema hili nitalifanya “labda kama si Kambarage!”

Daima alizungumzia matatizo ya nchi na suluhisho lake kwa namna iliyoonyesha kuwa aliamini umma una majibu ya matatizo yake kuliko kumtegemea yeye kiongozi. Na alipohisi kuwa umma unamtegemea kiongozi, alishtuka na kuanza kuelimisha watu.

Mara mbili alijiuzuru ukuu wa dola ili aende kwa wananchi kuwafanya wamiliki chama na kukipa nguvu. Alisisitiza daima kuwa nguvu ya chama ni  wanachama, si ya viongozi wala vyombo vya dola.

Ni baba huyu huyu hata baada ya kustaafu aliwahi kusema CCM si mama yake. Alisisitiza kuwa kwake chama ni sera na misingi. Kikiacha sera na misingi iliyokijenga, anakiacha. Aliendelea kuyasimamia haya mpaka mwisho wa maisha yake.

Mpaka wakati anakufa aliendelea kusema kuwa CCM kimeacha misingi yake, na kuwa kimegeuka kuwa chama cha viongozi na matajiri. Msimamo wake huu ulikuwa tishio kwa chama na viongozi wake, na walio katika kundi hilo kwa kweli walipata nafuu alipofariki.

Kuuawa kwa Azimio la Arusha na kuanzishwa kwa Azimio la Zanzibar vilimkera sana.

Sasa tuna Magufuli. Hata yeye bila aibu wala chembe ya kusita anasema “CCM ya Magufuli” itafanya hiki na kile. Nimemsikia kada mmoja pale ofisi ndogo ya CCM Lumumba akidai kirefu cha CCM kibadilishwe na kuwa “Chama Cha Magufuli.”

Nilipomuuliza kwa nini, akasema, Mwenyekiti mpya ana agenda mpya inayoweza kuiua CCM hii iliyopo na kuzaa CCM yenye “M” ya Magufuli. Alikuwa anatania lakini kwa nafasi yake, hakupaswa kufanya utani wa hatari kama ule.

Ukitafakari kwa makini unaweza kuona ukweli uliomo katika utani wa kada huyo. Magufuli haachi mwanya wa kuona tofauti yake na ya chama. Chama kinaonekana kuwa yeye, na yeye kuwa ni chama.

Nimesikia kuwa mwenyekiti Magufuli baada ya kuteuliwa kuwa mgombea wa urais wa CCM aliwaita baadhi ya wazee waliokuwa wamekata tamaa na CCM na kuwataka warudi katika chama kwa sababu yeye binafsi atakisafisha.

Baada ya kukabidhiwa uenyekiti, tumeshuhudia baadhi ya makada waliokuwa upinzani, wakirejea tena CCM kumfuata Magufuli. Huu ni mtazamo wa hatari sana kwa sababu unakimilikisha chama mikononi mwa mtu mmoja aitwaye Magufuli. Vyombo vyake kama NEC na CC havina nafasi tena katika maamuzi.

Magufuli ni mwepesi wa kuomba huruma nyepesi kwa wananchi na mwenye hulka ya kutukuzwa kwa ubabe wake wa kufanya maamuzi. Nilionya huko nyuma juu ya hatari ya kuunganisha kofia lakini nikapuuzwa. Kinachoweza kutokea sasa ni cha hatari zaidi.

Chama huongozwa na imani, si nguvu za dola. Hivi sasa hata ndani ya chama, hofu imetanda ya kushughulikiwa na vyombo vya dola. Magufuli amejizungusha na wakuu wa vyombo vya dola (usalama wa taifa, polisi na jeshi la wananchi), na hawa ndiyo wanampa ushauri wa namna ya kuendesha nchi na kuongoza chama.

Kada yule yule wa Lumumba amenishtua pale aliposema “hata kuteuliwa kwake kupeperusha bendera ya CCM kuliridhiwa na wenye nyota begani kwanza.” Haya kama si uzushi ni maneno ya hatari. Kama ni uzushi, ni imani ya hatari kwa nchi na kwa CCM. Kwa nini?

Taifa letu ni la kidemokrasia. Haliwezi kuongozwa na majeshi yaliyojificha nyuma ya rais na mwenyekiti wa chama tawala. Kufanya hivyo ni kujihatarisha yeye mwenyewe na kuhatarisha amani ya nchi.

Siasa na majeshi inapaswa iwe kama moto na petroli. Kama magufuli anafanya hivyo kwa kutaka kuvikomoa vyama vya upinzani, anadanganyika sana. Namshauri ateua haraka mshauri wa mambi ya siasa ili ampe shule ya kuyaondoa majeshi katika masuala ya kisiasa kwa usalama wake  mwenyewe na nchi yetu. CCM ndiyo iliyopeleka rushwa serikalini.

Ni CCM iliyopeleka rushwa na ufisadi majeshini. Ni kitu gani kinamdaganya Magufuli kuamini kuwa majeshini kuna watu wasafi wasio na tamaa ya utajiri na madaraka?

…………………………………………………………………………………………………..

Soma gazeti la MwanaHALISI kila Jumatatu kwenye simu yako kupitia, (bonyeza)> Mpaper kwa wateja wa Vodacom pia (bonyeza)> Simgazeti kwa wateja wa Vodacom, Tigo na Airtel. Pia unaweza kupakua (download) app ya Mpaper au Simgazeti kutoka kwenye playstore.

error: Content is protected !!