August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM chali tena Dar

Spread the love

VYAMA vinavyoundwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimezidi kukinyima raha Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndani ya Jiji la Dar es Salaam baada ya kukibwaga tena katika kinyang’anyiro cha Naibu Meya wa Jiji, anaandika Happiness Lidwino.

Katika uchaguzi wa Naibu Meya wa Jiji uliofanyika katika ukumbi wa Karim Jee Dar es Salaam mgombea CCM Mariam Lulida aligaragazwa na mgombea wa Ukawa Mussa Kafana kutoka Chama Cha Wananchi (CUF) kwa kura 16.

Akitangaza matokeo ya wagombea hao baada ya kura kupigwa Sarah Yohana Kaimu Mkurugenzi wa Jiji amesema jumla ya wapiga kura ni 16,zilizoharibika ni sifuri, kura halali ni 16, hivyo Kafana amepata kura 10 huku Lulida akipata kura 6.

Kafana ambaye pia ni diwani wa Kiwalani baada ya kuapishwa na Aziza Kalli Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive Dar es Salaam amewashukuru wapiga kura wake kwa ujumla huku akikishukuru chama chake na viongozi wa Ukawa kwa kufanya kazi kwa ushirikiano.

Baada ya kiapo Kafana ameahidi kushirikiana na Isaya Mwita Meya wa Jiji katika kuleta maendeleo huku akiahidi kuborsha vitu vyote ambavyo haviko sawa hususani mali za wananchi.

Katika hatua nyingine Kafana ameahidi kufanya kazi kwa umoja bila kujali itikadi za vyama huku akisema atakuwa mstari wa mbele katika kumshauri Mwita katika maamuzi ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kuboresha mambo yanayominya haki za wananchi.

“Niwatoe hofu wananchi wote waliotupigia kura kuwa, timu walioichagua kukamata Jiji hili ni nzuri, haibabaishwi wala kutishwa kwa kuwa inajiamini na ipo tayari na itaweza kukumbizana na kasi ya Rais John Magufuli” amesema Kafana.

Naye Lulida ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mchafukoge licha ya kushindwa kupata kiti cha unaibu Meya amesema, “Nitashirikiana na mwenzangu aliyepata nafasi hii nitajitaidi kumpa mawazo chanya ili kuboresha kwani lengo letu wote ni kuwahudumia wananchi”.

Naye Abdallah Chaurembo Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke akitoa maoni yake juu ya uchaguzi huo wa Naibu Meya amesema, “Kwakweli uchaguzi ulikuwa wa haki na huru, hakuna aliyeonewa wala kuibiwa na tumeridhika na matokeo kwani lengo ni moja kuwasaidia wananchi.”

error: Content is protected !!