May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CAG: Nyaraka za kughushi zilitumika Jeshi la Zimamoto

Thobias Andengenye, Mkuu wa jeshi la zimamoto

Spread the love

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema, nyaraka za fedha za kughushi zimetumika katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kuisababisha hasara serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Amesema, ukaguzi wake kwa mwaka 2019/2020, umebaini akaunti ya masurufu ya jeshi hilo, ilitumika kupitisha malipo batili ya Sh. 261.35 milioni.

Mdhidbiti huyo ametoa taarifa hiyo leo Alhamisi tarehe 8 Aprili 2021, wakati akitoa muhtasari wa ripoti ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020, jijini Dodoma.

“Nilibaini Sh. 261.35 milioni ziliwekwa kwenye akaunti ya masurufu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, katika mojawapo ya benki za biashara kwa vipindi tofauti.”

Charles Kichere, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)

“Hata hivyo, Menejimenti ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji haikutambua vyanzo vya fedha hizo na hakukuwa na mawasiliano yoyote yaliyofanywa na benki kuhusuiana na mapokezi ya fedha hizo,” amesema CAG Kichere.

Sambamba na hilo, CAG Kichere amesema, katika ukaguzi wake, alibaini kwamba, kiasi cha fedha hizo zilitolewa na mtunza fedha wa jeshi hilo, kwa kutumia nyaraka za fedha za kughushi.

“Pia, nilibaini kuwa, Kiasi hicho cha fedha kilichukuliwa na mtunza fedha wa Jeshi kutoka katika akaunti hiyo kwa vipindi tofauti, kwa kutumia nyaraka za fedha za kughushi,” amesema CAG Kichere.

Aidha, CAG Kichere amesema alibaini kuwa, usuluhishi wa taarifa za benki kwenye akaunti ya masurufu ya jeshi hilo, haukufanywa kuanzia tarehe 1 Julai 2019 hadi tarehe ya kukamilishwa kwa ukaguzi huo.

“Hii ni kinyume na Kanuni Na. 162 (1) ya Kanuni ya Fedha za Umma ya mwaka 2001 ambayo inahitaji taarifa za fedha za benki, zifanyiwe usuluhisho angalau kila mwezi.

“Hali hii inaashiria udhibiti dhaifu wa mifumo ya ndani kwenye usimamizi wa fedha katika akaunti za benki za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,” amesema CAG Kichere.

error: Content is protected !!