SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL), limetengeza hasara katika kipindi cha miaka mitano, ambapo mwaka huu, limetengeza hasara ya Sh. 60 bilioni. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumapili tarehe 28 Machi 2021, na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, wakati anawasilisha ripoti yake ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020, Ikulu jijini Dodoma.
CAG Kichere amewasilisha ripoti hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Shirika letu la ndege nimegundua limetengeza hasara , mwaka huu limetengeza hasara Sh. 60 bilioni, lakini kwa miaka mitano limekuwa likitengeneza hasara pia,” amesema CAG Kichere.
CAGKichere amesema hayo wakati anaeleza muhtasari wa ukaguzi uliofanywa katika mashirika ya umma, ambapo amesema pia, amebaini ubadhirifu katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Mdhibiti huyo na mkaguzi wa hesabu za serikali amesema ofisi yake inaendelea kukagua ubadhirifu huo, huku akiiomba Serikali ya Rais Samia kuzifanyia kazi changamoto hizo.
“Ukaguzi tuliofanya katika mashirika mbalimbali ya Serikali, tumegundua changamoto kadhaa ambazo zinahitaji serikali kukagua, ikiwemo matatizo katika Shirika la Bandari, ubadhirifu ambao tunaendelea kufanya ukaguzi katika maeneo hayo,” amesema CAG Kichere
Leave a comment