MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ameonesha wasiwasi wa upotevu wa mapato ya serikali ya Sh. 2.60 Bil katika Kivuko cha Magogoni (Kivuko cha Kigamboni), mkoani Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
CAG Kichere ameonesha wasiwasi huo leo tarehe 8 Aprili 2021, wakati akitoa muhtasari wa ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020, jijini Dodoma.
Akielezea ukaguzi wake alioufanya katika Wakala wa Ufudni na Umeme (TEMESA), amesema unaosimamia kivuko hicho, mfumo wake wa tiketi za kielektroniki hauna udhibiti wowote, na kwamba tiketi zaidi ya milioni 12 zenye thamani ya Sh. 2.60 Bil hazikuthibitishwa (scanned) katika mfumo uliopo.
Mkaguzi huyo amesema, tiketi hizo ni kati ya tiketi milioni 21.44 zenye thamani ya Sh. 5.76 Bil zilizotolewa na kituo hicho kuanzia Januari 2019 hadi Juni 2020.
“Pale pia tulikuta mfumo usio madhubuti katika tiketi za kielektroniki katika kituo cha feri Magogoni, nimebaini kuwa TEMESA imeuza tiketi Mil 21.447 zenye thamani ya Sh.5.76 Bil, hata hivyo tiketi Mil. 9.12 tu zenye thamani ya Sh. 3.6 Bil ndio zilithibitishwa na mashine (scanned).
“Hivyo, jumla tiketi milioni 12.3 zenye thamani ya Sh. 2.60 Bil, zikitumika bila kuthibitishwa. Wasiwasi wetu ni kwamba hizi tiketi zinaweza kutumika mara mbili na kusababisha upotevu wa mapato ya serikali,” amesema CAG Kichere.
Mbali na hilo, CAG Kichere amesema, makusanyo ya kivuko hicho Sh. 81.194 milioni, hayakuwasilishwa katika akaunti ya benki ya TEMESA, hadi ukaguzi huo unafanyika.
“Makusanyo ya kivuko ambayo hayajapelekwa benki na hayako kituoni ni Sh. 81.194 Mil. Hayo makusanyo yalifanyika katika kituo cha kivuko pale. Jumla yalikuwa Sh. 5.75 Bil ikiwa ni tozo ya kivuko kuanzia tarehe 1 Julai 2019 hadi 30 Juni 2020,” amesema CAG Kichere na kuongeza:
“Kati yake zilizokusanywa Sh. 5.6 Bil ndizo ziliwekwa katika akaunti ya benki inayosimamiwa na TEMESA, ukiacha Sh. 81.194 Mil ikiwa bado hazijawekwa benki hadi muda wa ukaguzi, nimebaini kisi hicho hakikuwa ndani ya himaya ya kituo, kuna uwezekano zilitumiwa vibaya au kwa shughuli nyingine.”
Leave a comment