Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CAG amweka pabaya waziri wa JPM bungeni
Habari za Siasa

CAG amweka pabaya waziri wa JPM bungeni

Spread the love
 HALIMA Mdee, Mbunge wa Kawe na John Mnyika wa Kibamba (wote Chadema) wamemkaria kooni Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango wakitaka kujua zipo wapi fedha zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Anaripoti Dany Tibason, Dodoma … (endelea). 

Mnyika na Mdee kwa pamoja walimtaka Dk. Mpango awaeleze Watanzania wapi wamezipeleka Sh. 1.5 trilioni, zilizotajwa na CAG.

Wakizungumza leo Juni 5 bungeni, wabunge hao wamemtaka CAG kufanya ukaguzi maalumu wa fedha hizo na deni la Taifa huku wakisema kama Dk. Mpango ameshindwa kuongoza wizara hiyo  ni bora akajiuzulu ili asiwe waziri wa fedheha.

Hoja hiyo imeibua mvutano bungeni kati ya wabunge  hao, Waziri Mpango na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akiwazuia kujadili ripoti hiyo ndani ya Bunge.

Akianza kuchangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya wizara ya fedha na mipango ya mwaka 2018/19, Mnyika amesema waziri wa fedha, Dk Mpango na taasisi zilizo chini yake, zinaandika barua kwamba mtu fulani asipewe msahama wa kodi halafu mlango wa nyuma anakwenda kutoa msamaha, kama sio fedheha ni nini?

Kauli hiyo ilimnyanyua, Dk Mpango ambaye  alisema; “Mheshimiwa Mwenyekiti (wa Bunge- Najima Giga) naomba (Mnyika) athibitishe hilo.”

Mnyika akiendelea kuchangia amesema kumekuwa na kawaida wizara ya fedha kutoa kauli humu bungeni zinazokinzana.

“Aprili 20, 2018 Naibu waziri wa fedha (Dk Ashatu Kijaji) alitoa kauli humu bungeni kuhusu utata wa Sh. 1.5 trilioni ambazo hazijulikanani zimeenda wapi. Akasema Sh. 209 bilioni zimepelekwa Zanzibar, nimefuatilia mjadala wa baraza la wawakilishi sijaona hilo, CAG achunguze na ufanyike ukaguzi maalum,” amesema Mnyika.

Baada ya kutoa kauli hiyo, Waziri Mhagama amesimama na kusema;  “Kauli za mawaziri, huwa hazijadiliwi bungeni, ninaomba nisisitize kauli za mawaziri hazijadiliwi bungeni.”

Waziri Mhagama amesema ripoti za CAG zitajadiliwa ndani ya Bunge mara baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuijadili na kuwasilisha taarifa yake ndani ya Bunge.

 “Kwa hiyo hapa ndani ya Bunge tutaenda na kanuni na kama ni kujadili nje ya bunge wako wabunge wengine watalijadili,”amesema.

Baada ya kumaliza, kelele ziliibuka kutoka upinzani wakipinga huku Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga akimtaka Mnyika kuendelea kuchangia.

“Lazima CAG akalifanyie uchunguzi maalumu suala la Sh 1.5trilioni na kuhusu vile vifungu namba 22 kuhusu  deni la Taifa,”amesema  Mnyika

Kwa upande wake, Mdee amesema taarifa ya CAG ni halali kwa wabunge  kulijadili.

Mdee amesema Waziri Mpango  anatakiwa  ajibu hoja kuhusu Sh. 1.5 trilioni na Sh. 200 bilioni zilizotajwa kupelekwa Zanzibar ni zipi?

Hata hivyo, Spika Job Ndugai alimtaka Mnyika kujiandaa kuthibitisha hoja yake kuhusu Dk. Mpango kuzuia msamaha wa kodi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!