Tuesday , 23 April 2024
Home Habari Mchanganyiko CAG abaini ‘madudu’ kwenye majeshi
Habari MchanganyikoTangulizi

CAG abaini ‘madudu’ kwenye majeshi

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) nchini Tanzania, Charles Kichere
Spread the love

 

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) nchini Tanzania katika ukaguzi wake kwa mwaka 2020/21 amebaini udhaifu wa usimamizi, ufuatiliaji na ukiukwaji wa sheria za ununuzi uliofanywa na taasisi mbalimbali likiwamo Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Pia, Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Magereza na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Ripoti hiyo ni inayoishia Juni 30 2021 ambayo CAG Charles Kichere aliiwasilisha bungeni Dodoma hivi karibuni inaonesha jinsi fedha za walipakodi zinavyotafunwa na wachache kwenye maeneo mbalimbali.

Katika ripoti ya Serikali Kuu, CAG Kichere amebaini malipo yenye shaka ya Sh mbilioni 1.38 kwenye ununuzi wa silaha za kijeshi ambazo hazijapokewa yaliyofanywa na Shirika la Mzinga lililo ndani ya JWTZ.

CAG Kichere alisema, tarehe 23 Novemba 2020, Shirika la Mzinga lilisaini mkataba na SMT Security Ltd juu ya ununuzi wa silaha za kijeshi kwa bei ya mkataba ya euro 572,444 sawa na Sh bilioni 1.61.

Alisema muda wa uwasilishaji silaha hizo ulikubaliwa kuwa Novemba 26, 2020.

Jenerali Venance Mabeyo, Mkuu wa Majeshi Tanzania

CAG alisema, alibaini kifungu cha 18 (ii) cha masharti maalumu ya mkataba, kinamtaka msambazaji alipwe malipo ya awali sawa na asilimia 50 ya bei ya mkataba na asilimia 35 ya bei ya mkataba baada ya kuwasilisha ushahidi wa usafirishaji mzigo.

“Hata hivyo, niligundua kuwa Shirika la Mzinga lilimlipa msambazaji jumla ya euro 486,577 (Sh bilioni 1.38) sawa na asilimia 85 ya bei ya mkataba, bila ushahidi wa upakiaji na usafirishaji silaha,” alisema CAG Kichere na kuongeza:

“Pia, nilibaini Shirika la Mzinga bado halijapokea silaha zilizolipiwa kutoka kwa msambazaji, ikiwa miezi 15 imepita tangu muda wa uwasilishaji silaha Novemba 26, 2020 hadi muda wa ukaguzi Februari 7, 2022.”

CAG alisema ingawa, Mzinga ilieleza janga la UVIKO-19 kama sababu kuu iliyoathiri uzalishaji na usambazaji silaha, “maoni yangu ni kuwa udhaifu huo ulichangiwa na mfumo usioridhisha wa udhibiti wa ndani wa Shirika la Mzinga.

“Udhaifu huo uliruhusu malipo kufanyika bila kuzingatia kifungu cha mkataba cha uwasilishaji ushahidi wa usafirishaji. Hivyo, hatua hiyo inaiweka Serikali katika hatari ya kupata hasara ikiwa msambazaji hatawasilisha silaha hizo,” alisema CAG Kichere na kuongeza:

“Napendekeza Shirika la Mzinga liimarishe mifumo ya udhibiti wa ndani, ili kuhakikisha vifungu na wajibu wa mikataba vinazingatiwa. Aidha, napendekeza Shirika la Mzinga kuhakikisha mwuzaji anawasilisha silaha zilizolipiwa bila kuchelewa zaidi.”

IGP Simon Sirro

Madeni makubwa

Katika ripoti hiyo, CAG alitaja taasisi 14 zenye madeni ya thamani ya juu ya muda mrefu ya Sh trilioni 3.61 na miongoni ni taasisi za majeshi, ambapo Shirika la Mzinga lina deni la Sh mbilioni 51.38 bilioni, JWTZ Sh bilioni 314.52 na Jeshi la Polisi Sh bilioni 641.79.

Zingine ni Wizara ya Ulinzi na Usalama wa Taifa Sh trilioni 1.01, Idara ya Magereza Sh bilioni 80.17, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Sh bilioni 25.8.

“Kushindwa kulipa madeni kwa wakati, kumeathiri vibaya sifa ya Serikali kwa wakandarasi, wauzaji na watoa huduma, huongeza gharama kutokana na riba na adhabu kwa malipo yanayolipwa kwa kuchelewa na kuongeza ziada ya bajeti,” alisema CAG.

Alisema changamoto anayoiona ni hali ya bajeti ya Serikali ambayo ipo katika msingi wa fedha taslimu, wakati uhalisia wake upande wa matumizi ni kwa msingi usio wa fedha taslimu.

“Kwa hiyo, naishauri Serikali itoe fedha kulingana na bajeti iliyoidhinishwa na kwa wakati, ili kupunguza wingi wa madeni ya muda mrefu yanayoambatana na riba na adhabu, wakati wa kulipa madeni hayo na kuweka madeni ya sasa katika bajeti za kila mwaka za taasisi husika,” alisema.

Polisi yalipa milioni 178/-

Ripoti hiyo ya CAG imebaini Kitengo cha Matengenezo cha Magari ya Polisi kilianzishwa mwaka 1969 kwa ajili ya matengenezo ya magari ya Polisi na pikipiki kwa upande wa Tanzania Bara.

Alisema katika mwaka wa fedha 2020/21, “nilibaini Sh milioni 178.21 zililipwa kwenye karakana binafsi kwa ajili ya kupata huduma ya matengenezo ya magari badala ya Kitengo cha Matengenezo cha Magari ya Polisi.

Kamishna wa Magereza, Meja Jenerali, Suleiman Mzee

“Hii ilitokana na sababu mbalimbali zikiwamo; mabadiliko kwenye teknolojia ya magari, watumishi kwenye kitengo kutopata mafunzo stahiki, kuibuka ujuzi mpya kwenye soko na kutokuwapo rasilimali stahiki na za kutosha,” alisema.

CAG Kichere alisema: “Ni maoni yangu, kushindwa kwa watumishi wa Kitengo cha Matengenezo cha Polisi kuwa na ujuzi na vifaa stahiki kunaweza kusababisha kwa kitengo kukosa umuhimu na kuifanya Serikali kuingia gharama zaidi za matengenezo ambazo zingeepukika.”

Akihitimisha kwenye eneo hilo, CAG Kichere alisema: “Nashauri Jeshi la Polisi likishirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha Kitengo cha Matengenezo cha Magari ya Polisi kina ujuzi na vifaa vya kutosha, ili matengenezo ya magari kwa siku za baadaye yafanyike kwa usalama na kwa gharama nafuu.”

Hali mbaya Magereza

CAG alisema, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, haisimamii na kutoa ipasavyo miundombinu ya mahabusu na magereza.

“Jeshi la Magereza halina uwezo wa kutosha kuboresha miundombinu ya mahabusu na magereza, kutokana na uhaba wa bajeti na watumishi,” alisema.

CAG Kichere alisema zaidi ya hayo, Wizara haina utaratibu madhubuti wa kuratibu na kufuatilia utendaji wake, na wa Jeshi la Magereza, ili kuongeza uwezo wa miundombinu ya magereza na hali ya mahabusu na wafungwa nchini.

Alisema hali hii ni kwa sababu malengo na mipango iliyowekwa ya kupunguza msongamano na utoaji huduma kwa magereza haijatekelezwa na kufikiwa ipasavyo na Jeshi la Magereza na Wizara ya Mambo ya Ndani.

“Hali ya magereza na vizuizi nchini bado ni mbaya, ambayo inahatarisha utu wa mahabusu na wafungwa,” alisema CAG Kichere.

CAG alisema utawala na utoaji miundombinu ya ruzuku na magereza unalenga lengo namba 16 la Malengo ya Maendeleo Endelevu.

“Ukaguzi huu umebaini upungufu katika uanzishaji na ukarabati wa miundombinu ya mahabusu na magereza, kwenye uhaba wa malazi ya mahabusu na wafungwa; uchakavu wa majengo na makazi ya askari; na uwezo mdogo wa taasisi zinazosimamia miundombinu ya mahabusu na magereza nchini,” alisema.

Alisema iwapo upungufu hautashughulikiwa ipasavyo, unaweza kuathiri ufikiaji wa lengo namba 16 la Malengo ya Maendeleo Endelevu, linalosisitiza uwapo wa jamii jumuishi zenye amani na umoja kwa maendeleo endelevu; kutoa nafasi ya haki kwa wote; na kujenga taasisi zenye ufanisi, zinazowajibika na jumuishi katika ngazi zote.

“Shabaha ya lengo hili ni kuwapo taasisi imara, ikiwa ni pamoja na kukuza utawala wa sheria katika ngazi ya kitaifa na kimataifa na kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wote,” alisema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Watuhumiwa 12 wa kilo 726.2 za dawa za kulevya wafikishwa mahakamani

Spread the love  WATUHUMIWA watatu wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Mkoani...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari Mchanganyiko

GGML yasisitiza kuendelea kuimarisha afya za wafanyakazi

Spread the loveKAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited kwa kushirikiana na kampuni...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!