RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), nchini Tanzania kwa mwaka 2019/20, imebaini kasoro kwa vyama vya siasa vikiwemo, Chadema na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).
Ripoti hizo za CAG, Charles Kichere zimewasilishwa jana Alhamisi tarehe 8 Aprili 2021, bungeni jijini Dodoma.
Kichere amesema, kwa mwaka wa fedha 2019/20, amepokea taarifa za fedha za vyama 17 kati ya vyama 19 vilivyosajiliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Chama cha Democratic Party (DP) na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) havikuwasilisha taarifa zao za fedha,” amesema Kichere.

CAG amesema, “Ofisi ya CCM Mkoa wa Mwanza, haikukusanya malipo ya kodi za pango Sh.348.46 milioni kutoka kwa wapangaji 149 wa kiwanja cha CCM Kirumba na Ofisi ya CCM ya Mkoa wa Mwanza.”
“Ukaguzi wangu, umebaini Ofisi ya CCM Lumumba, Dar es Salaam ilitumia Sh. 27.09 milioni kwenye ununuzi wa bidhaa na huduma bila ya kufuata taratibu za ushindani za ununuzi.”
Kichere amesema ,”Ofisi ya CCM Zanzibar ilinunua bidhaa za jumla ya Sh.75.05 milioni na kulipa taslimu kwa wazabuni badala ya kuhamisha malipo hayo kwenye akaunti zao za benki.”
CAG huyo amesema, “Chadema kilinunua magari matano yenye thamani ya Sh. 227.43 milioni na nyumba moja Sh. 50 milioni iliyopo Serengeti bila idhini ya Baraza Kuu la Chama. Pia, Sh.100 milioni zilitumika kwenye matumizi ya kawaida ya chama bila ya idhini ya baraza kuu la chama.”

Pia, chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania “kilifanya malipo yasiyokuwa na tija Sh. 19.8 milioni kulipa bakaa ya mkopo wa mmojawapo wa viongozi wa chama hicho aliyeacha uanachama wa Chadema.”
Kichere amesema, Chama Cha Wananchi (CUF), “kilituma kiasi cha Sh.72.98 milioni kwa mmoja wa wanachama wake kwa ajili ya ununuzi wa magari mawili kutoka kwa mojawapo wa wazabuni waliopo Japani.”
“Mwanachama huyo alinunua magari hayo na yalisajiliwa kwa majina binafsi badala ya jina la Baraza la Wadhamini la CUF,” amesema
Ndani ya chama hicho, CAG Kichere amesema “nilibaini kuwa CUF kinamiliki magari tisa na pikipiki 27 ambazo zina majina ya watu binafsi badala ya jina la Baraza la Wadhamini la CUF.”
“Chama cha Wananchi (CUF) kilidai kumiliki magari 24 na pikipiki 24 ambazo zilikuwa zikitumika Zanzibar. Hata hivyo, hakukuwa na ushahidi wa kuthibitisha umiliki huo,” amesema
CAG amesema “nilibaini utata kwenye umiliki wa magari sita na aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi kutokana na hoja zifuatazo: Sikuweza kuhakiki Chanzo cha Dola za Marekani 85,637 zilizotumika kwenye ununuzi wa gari hizo.”
“Nilibaini kuwa magari hayo yalinunuliwa na Mkurugenzi huyo wa Fedha na Uchumi na kuyakabidhi kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) licha ya kukana saini yake. Nilibaini kuwa magari hayo yalisajiliwa kwa majina ya watu binafsi,” amesema
CAG amesema, vyama vya siasa 11 vilitumia jumla ya Sh. 347.52 milioni bila ya kuwa na nyaraka toshelezi. Hivyo, sikuweza kuhakiki sababu, uhalali na uhalisia wa malipo yaliyofanyika.
“Vyama vya siasa vitano vilichelewa kuwasilisha taarifa zao za fedha kwa ajili ya ukaguzi kwa kipindi kati ya siku 42 hadi 126.”

Kichere amesema “vyama vya siasa kumi viliandaa taarifa zao za fedha bila ya kufuata kwa mfumo wa kimataifa wa uandaaji wa taarifa za fedha (IPSAS) kama ilivyoanishwa kwenye Kanuni Na. 3(1) ya Kanuni za vyama vya Siasa (uhasibu wa fedha) za mwaka 2019.”
Amesema, vyama vya siasa vinane vilitumia mapato yake yaliyopokelewa ya jumla ya Sh. 244.58 milioni bila kuwekwa benki kinyume na Kanuni Na. 15(1) ya Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 iliyorejewa mwaka 2019.
CAG amesema, Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) na Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) havikuandaa tamko la mali na kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kinyume na Kifungu Na. 14(1)(ii) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 iliyorekebishwa mwaka 2019.
Amesema, Chama cha UMD, Chama cha UDP, Chama cha NCCR-Mageuzi na Chama cha Demokrasia Makini, havikuhuisha rejista za wanachama na viongozi wake, kinyume na Kifungu Na. 8C cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 iliyorejewa mwaka 2019.
“Chama na Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) hakikuwasilisha ritani ya mwaka ya wajumbe wa Baraza la Wadhamini toka mwaka 2006, kinyume na Kifungu Na. 16(3) cha Sheria ya Usajili wa Udhamini Sura ya 318,” amesema
Leave a comment