Spread the love

OFISI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imebaini kiasi cha Sh bilioni 22.64 kilichohamishwa kutoka makao makuu ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuelekea bandari ya Mwanza, hakikuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu maombi ya kuhamishwa kwa fedha hizo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Pia katika uchunguzi maalumu uliofanywa na CAG katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015 hadi 2020, amebaini kukosekana kwa ushahidi wa idhini ya kuhamisha fedha Sh bilioni 24.29 zilizopelekwa Bandari ya Mwanza.

Hayo yamebainishwa katika Ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma ya mwaka 2020/2021 iliyowasilishwa bungeni jana tarehe 12 Aprili, 2022 na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere.

Ubadhirifu huo umeanikwa kutokana na ukaguzi maalum wa taarifa za benki zilizowasilishwa na uongozi bandari ambapo CAG alibaini kuwepo kwa miamala 157 yenye thamani ya jumla ya Sh bilioni 34.67 ya kuhamisha fedha kutoka Makao Makuu ya TPA kwenda Bandari ya Mwanza kuanzia mwezi Januari 2015 hadi Machi 2020.

Akifafanua kuhusu kukosekana kwa ushahidi wa maombi ya kuhamishwa fedha Sh bilioni 22.64 zilizotumwa Bandari ya Mwanza, CAG amesema kati ya miamala 157 ya kuhamisha fedha, menejimenti ilimpa nyaraka za maombi ya kuhamisha fedha kwa miamala 51 yenye thamani ya shilingi bilioni 12.03 wakati miamala yenye thamani ya shilingi bilioni 22.64 haikuwa na nyaraka za maombi ya kuhamisha fedha zilizoletwa kwangu kwa ajili ya uhakiki.

Kuhusu kukosekana kwa ushahidi wa idhini ya kuhamisha fedha Sh bilioni 24.29 iliyotumwa kuelekea Bandari ya Mwanza, CAG amesema kati ya miamala 157 ya kuhamisha fedha, menejimenti ilimpatia uthibitisho wa vibali 49 vilivyoidhinisha fedha zilizotumwa bandari ya Mwanza wakati miamala yenye thamani ya shilingi bilioni 24.29 haikuwa na vibali.

Pia alibaini kiasi cha Sh milioni 907.33 kiliidhinishwa zaidi ya kiasi kilichoombwa.

Charles Kichere

“Nilibaini kuwa, kati ya vibali 49 vya kuhamisha fedha, ni vibali 27 tu ndivyo vilikuwa na maombi ya fedha taslimu kutoka Bandari ya Mwanza vyenye jumla ya shilingi bilioni 1.187.

“Hata hivyo, nilibaini kuwa fedha zilizoidhinishiwa kuhamishwa kutoka TPA kwenda Bandari ya Mwanza ni Sh bilioni 2.095 badala ya kiasi kilichoombwa Sh bilioni 1.187, hivyo kuwapo na ziada ya Sh milioni 907.33,” amesema CAG kupitia ripoti hiyo.

Aidha, alibaini kuwa fedha Sh bilioni 2.09 zilizohamishiwa Bandari ya Mwanza zilizidi kiasi kilichoidhinishwa.

Amesema fedha taslimu zilizohamishiwa Bandari ya Mwanza zilikuwa Sh bilioni 2.89. Hata hivyo, nilibaini Sh milioni 812.78 pekee ndizo ziliidhinishwa kuhamishiwa Bandari ya Mwanza.

“Hivyo, kiasi kilichohamishiwa katika Bandari ya Mwanza kilikuwa kimevuka kiasi kilichoidhinishwa kwa Sh bilioni 2.09. Kiasi hiki cha ziada kilichohamishwa cha Sh bilioni 2.09 zilifanyiwa ubadhirifu na maofisa wa Bandari ya Mwanza.

“Mapungufu haya yanaashiria udhaifu katika udhibiti wa ndani ili kuhakikisha fedha hazihamishwi kwenda bandari husika zaidi ya zile zilizoidhinishwa,” amesema.

Kutokana na ubadhirifu huo CAG amependekeza (TPA) ihakikishe wahusika wanarejesha fedha zilizofanyiwa ubadhirifu pili ipitie upya mchakato wa uhamishaji wa fedha za Mamlaka kwa madhumuni ya kuimarisha udhibiti.

Pia katika uchunguzu huo alibaini ubadhirifu wa fedha kwa kutoa fedha taslimu Sh bilioni 8.38 katika Bandari ya Mwanza.

“Nilipitia taarifa za fedha za benki kutoka kwenye akaunti ya benki ya matumizi ya Bandari ya Mwanza kwa kipindi cha muda wa miaka mitano na miezi mitano kuanzia tarehe 1 Januari 2015 hadi 31 Machi 2020.

“Katika mapitio yangu nilibaini jumla ya hundi 7,888 zilitumika kutoa fedha Sh bilioni 31.76 kutoka benki kwa mujibu wa taarifa ya akaunti ya benki. Kati ya hundi zilizotumika kuchukua fedha zenye thamani ya Sh bilioni 31.76, ni hundi 4,777 tu zenye thamani ya Sh bilioni 19.41 ndizo ziliwasilishwa kwangu na Benki ya CRDB mnamo tarehe 30 Novemba 2020 kwa ajili ya ukaguzi.

“Hundi hizo 4,777 zilizopatikana ni pamoja na hundi 2,043 zenye thamani ya Sh bilioni 8.38, ambazo ziligongwa muhuri wa “lipa fedha taslimu” na kusainiwa nyuma yake na mlipwaji,” amesema.

Amesema hundi hizo 250 zilitumika kutoa fedha taslimu katika akaunti ya matumizi ya Bandari ya Mwanza bila kuandaliwa vocha za malipo kinyume na Kifungu cha 4.9.3(a) cha Kanuni za Fedha za Mamlaka ya Bandari Tanzania za Mwaka 2012.

“Kwa hiyo, malipo ya hundi 2,043 yalikuwa batili kwa kuwa yote hayakuwa na vibali vya miamala na ushahidi wa nyaraka za matumizi (vocha za malipo, na ankara/hati za madai zilizoambatanishwa),” amesema.

Amesema licha ya kwamba TPA ilikuwa na watiasaini watatu, alibaini kuwa hundi zote 2,043 zilizolipwa kwa miaka mitano na miezi mitatu zilisainiwa na watiasaini wawili.

“Mmoja wa watiasaini, kupitia baruapepe ya tarehe 7 Januari 2021 alithibitisha kuwa kiasi cha shilingi bilioni 8.38 kilitolewa bila kuwa na vocha za malipo na nyaraka zingine.

“Ninapendekeza kuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (a) ihakikishe watumishi waliohusika wanarejesha fedha shilingi bilioni 8.38; na (b) ifanye uchunguzi wa hundi 3,111 ambazo hazikuwasilishwa kwangu na benki,” amesema CAG.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *