May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CAF waridhia ombi la Simba, mechi kuchezwa saa 11            

Haji Manara, Msemaji wa Simba

Spread the love

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeridhia ombi la klabu ya Simba kuchezwa kwa mchezo wao dhidi ya FC Platinum kuchezwa majira ya saa 11 jioni badala ya saa 1 usiku kama ilivyokuwa hapo awali. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Mchezo huo wa marudiano wa klabu bingwa barani Afrika utapigwa siku ya Jumatano tarehe 6 Januari, 2021, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, huku Simba akiwa amepoteza kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Zimbabwe kwa bao 1-0.

Akiongea mbele ya waandishi wa habari hii leo tarehe 4 Januari, 2020 kwenye Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, Haji Manara alisema kuwa hapo awali mchezo huo CAF walipangwa uchezwe saa 1 usiku ila kama klabu tukaomba muda wa mchezo huo urudishwe kutokana na miundombinu pamoja na mazingira wanayotokea mashabiki wetu.

“CAF wameridhia ombi letu la mchezo wetu dhidi ya Platinum kuchezwa saa 11 jioni, tofauti na ilivyopangwa awali kuchezwa saa 1 usiku,” alisema Manara.

Manara alisema wapinzani wao wameshafika nchini na kesho watafanya mazoezi kwenye Uwanja utakaochezewa mechi kama ilivyo kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo.

“Mechi itakuwa Jumatano kwenye Uwanja wa Mkapa, saa 11 jioni na wageni wetu timu ya Platinum imeshafika na wanaendelea na maandalizi yao na kesho watafanya mazoezi kwenye Uwanja huo,” aliongezea Manara.

Aidha Manara alitumia wasaa huo kuwataka mashabiki na wapenzi wa klabu ya Simba kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo ili kuweza kuwapa hamasa wachezaji kwa kuwa waoa wanaamini mtaji wao ni mashabiki licha ya kuruhusiwa kuingiza asilimia 50 ya mashabiki.

“Tulitamani idadi ya watu ifike vile tunavyotaka kutokana na mtaji wetu mkubwa ni mashabiki na tunaamini watatuunga mkono pamoja na kutusapoti ili kuwapa hamasa wachezaji wetu.

“Sisi tuliomba CAF tujaze uwanja wote lakini mpaka sasa hatujajibiwa na itaendelea kubaki asilimia 50 kama ilivyokuwa hapo awali ila tukijibiwa ombi letu tutafanya hivyo,” alinena Manara.

Kama Simba ikifanikiwa kushinda mchezo huo itakuwa inafuzu kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Klabu Bingwa kama ilivyofanya kwenye msimu wa 2018/19 baada ya kuwaondosha Nkana kutoka Zambia na kama ikitokea Simba kupoteza mchezo huo itakwenda kwenye kombe la shirikisho barani Afrika.

Viingilio vya mchezo huo tayari vimeshawekwa wazi ambapo kima cha chini kitakuwa 5,000 kwa mzunguko, Vip B na C itakuwa Sh. 15000 huku Vip A, ikiwa Sh. 20,000.

Simba inaingia kwenye mchezo huo huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 lililofungwa na Perfect Chikwende kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika nchini Zimbabwe.

error: Content is protected !!