July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Butiku: CCM magwiji wa rushwa

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku

Spread the love

JOSEPH Butiku, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), ameapa kufikia kwenye ukweli. Anasema yuko tayari kupoteza maisha kwa kutetea kile anachokiamini.

Alisema, “…mimi na Warioba (Jaji Joseph Sinde Warioba), tutaendelea kusema ukweli na njooni mtuchinje. Tutawaambia ukweli na tutasimamia ukweli huo.” Anaandika Jimmy Mfuru … (endelea).

Akizungumza katika mdahalo ulioitishwa na tasisi hiyo jijini Dar es Salaam mchana, Butiku alisema, “Ninawashangaa wazee kuingia kwenye makundi ya kusaka urais” na kuhoji, “kwa staili hiyo nani atamshauri rais katika uteuzi?”

Butiku alitoa kauli hiyo katika kongamano lililolenga kujadili amani katika kuelekea uchaguzi mkuu wa oktoba mwaka huu.

Amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndiyo vinara wa uvunjaji wa katiba na ununuzi wa kura katika chaguzi.

Alisema, “CCM ndiyo chama kinachoongoza kwa kutoa rushwa nchini wakati wa uchaguzi. Hivi sasa, wagombea wake wa urais wanazunguka mikoani, kutoa rushwa kwa lengo la kutafutwa uungwaji mkono.”

Alisema, “…vitendo vinavyofanywa na chama hiki, ni uvunjifu wa misingi ya amani na utulivu.”

Amesema rushwa ilianza rasmi ndani ya chama hicho mwaka 1995, wakati kulipoundwa mtandao wa kusaka urais, nje ya taratibu.

Alisema, “Hiki ni chama cha mizengwe. Ni chama cha fitna na majungu; ndivyo ambavyo waliokuwa wanatafuta madaraka wakati huo walivyohubiri mwaka 1995” na hatimaye wakafanikiwa kushika dola miaka 10 baadaye.

Akiongea huku akimtolea macho, Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Sinde Warioba, Butiku ilisema, “…bila kumumunya maneno nitawaambia kilichotokea mwaka 1995. Chama kilikuwa hakifuati taratibu na ni magwiji wakubwa wa kuvunja katiba na kuhonga.”

Alisema, “vijana waliunda mtandao ambao uliamua kufanya kazi nje ya taratibu ya chama. Wakajipanga kushika uongozi na kusema CCM ni chama cha mizengwe na kinawachelewesha kupata maendeleo hasa kutajirika kupitia madaraka ya umma.”

Butiku hakutaja waliounda mtandao wa kusaka madaraka. Lakini waliounda mtandao mwaka 1995, walikuwa ni Jakaya Kikwete, Rostam Aziz na Edward Lowassa.

Mtandao huu ulidumu hadi mwaka 2005, ambako uliimarika kwa kuingizwa Bernard Membe, Samwel Sitta na vijana wengine, wakiwamo Emmanuel Nchimbi.

Butiku ambaye alianza kutoa mada yake kwa kusema leo siyo siku nzuri kwake. Hana amani na utulivu moyoni kwa kuwa anashuhudia taifa linayumba na linapoteza misingi ya amani.

error: Content is protected !!