April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Buriani Kaka Evod Herman Mmanda

Marehemu Evod Mmanda

Spread the love

EVOD Mmanda, naomba uamke kaka yangu. Umeondoka mapema mno kaka. Kwa nini lakini? Anaandika Moses Machali … (endelea)

Kwangu hukuwa rafiki tu, bali Kaka wa kweli uliyependa kushauriana nami mambo mbalimbali. Daima hukuniacha katika mapito mbalimbali; magumu na mepesi.

Leo umelala mazima. Hata siamini! Ni jana Jumapili ya tarehe 26 Aprili 2020, nilikutumia ujumbe usemao:

“Kaka Mmanda,

Pole ndugu yangu. Vipi maendeleo lakini?” Ilikuwa majira ya saa 9 Alasiri, lakini ujumbe haukujibiwa, kumbe ulikuwa umezidiwa ukiwa katika hali ya mateso huku madaktari na wauguzi wakihangaika kupigania afya yako.

Wewe kaka Evod Mmanda hatukukutana Mtwara tu bali tangu enzi zile za vikao mbalimbali vya Tanzania Center for Democracy (TCD) na Bunge Maalumu la Katiba (BMK). Moyo wangu unaniuma sana leo kuona ukiwa umelala huwezi kujigeuza wala kuamka.

Wewe kaka ulikuwa mtu muungwana sana, mpole, mnyenyekevu na mvumilivu pia katika mengi.

Ulikuwa mshauri na mfariji wa watu tuliobahatika kuwa karibu yako. Leo umeondoka kaka yangu. Kwa nini imekuwa hivyo? Ni mapema mno na nashindwa kuamini?

Nakumbuka nilipofika Mtwara kuripoti kikazi ile tarehe 05 Agosti 2018, tulionana pale Mtwara Airport tukasalimiana na kukumbushana historia yetu ya nyuma. Tulichekeshana na kufurahi sana siku hiyo maana ilikuwa muda umepita pasipo kukutana tangu tulipoachana kwenye Bunge Maalumu la Katiba.

Ulinikaribisha vizuri sana Mtwara na kuniongoza katika mengi kaka Mmanda hususani katika Kazi ya Ukuu wa Wilaya tukiongozwa na Senior DC Seleman Mzee.

Wewe kaka Mmanda uliyeondoka leo na kuniacha nalia, kwangu ulikuwa Mwalimu katika majukumu ya ukuu wa wilaya. Hii inatokana na ukweli kwamba ulinitangulia kuwa mkuu wa wilaya na ulinipokea vizuri Mtwara.

Kuna nyakati nilikuwa nilikuwa nikikueleza ni jinsi gani ulivyokuwa msaada kwangu pamoja na akina Selemani Mzee, Aziza Mangosongo, na Mhe Sebastian Waryuba wa kule Tandahimba katika kuniongoza. Wewe na hao waheshimiwa wakuu wa wilaya wenzangu hamkuniacha hadi leo hii unapoondoka kaka.

Kama unaweza naomba uamke Mhe Mmanda. Umetuachia simanzi ndugu yangu. Hivi kweli ndiyo tumeagana mazima katika dunia hii? Hivi siku ile nilipokuja ofisini kwako wiki jana siku ya Jumatatu tarehe 20/04/2020 ndiyo ilikuwa tunaagana LIVE kwa Mara ya mwisho?

Ulikuwa ukipigania Afya yako kwa kuomba ruhusa na kwenda Muhimbili na Regency Dar es Salaam kwa nyakati tofauti. Leo umeondoka kaka. Kweli umeondoka ndugu yetu? Hautazungumza nasi tena? Hata siamini kabisa.

Anyway inanipasa niamini kwamba umeshatutoka na kilichobaki nikukuombea kwa Mola wetu akupokee katika ufalme wake. Akusamehe makosa pale ulipojikwaa na akuhifadhi mahala pema peponi.

Kaka Mmanda, naomba unifikishie salaam zangu kwa akina Nyerere, Edward Sokoine, Samuel John Sitta, Mzee wangu Joseph Machali, Mandela, Malcolm X, Robert Mugabe, Patrice Lumumba, Kwame Nkrumah, Lucky Dube, Bob Marley, Socreates, Martin Luther king Jr.

Vilevile, wasalimu sana akina Sylvester Willium Dubois, Marcus Moziah Garvey, akina Dr Edmund Sengodo Mvungi, Hayati Karume.

Pia usisahau kumsalimia Muamar Gaddafi wa kule Libya aliyependa kuiona Afrika akiwa moja na kujikwamua katika minyororo ya kuporwa na wazungu.

Waeleze viongozi wetu hao kwamba sisi Tanzania chini ya Rais Magufuli bado tunapambana kuijenga Afrika yenye nidhamu na inayojitegemea kiuchumi, Kisiasa na Kijamii. Mapambano bado ni mazito na hatutaacha kuyafanya. Ndoto zao bado zinaishi.

Wachache tunayo matumaini kwamba siku moja Afrika huru na Afrika Moja itapatikana. Uwepo wa Viongozi aina ya JPM mwenye element za akina Nyerere, Mandela na wengine katika miaka hii ni ishara na heshima kwetu PANI AFRICANISTS wa sasa. Tutaendeleza harakati zao.

Kaka Mmanda, naomba usiache kufikisha salam hizo kwa watu hao. Utakutana nao watu hao mashuhuri hapa duniani lakini jua umetuachia huzuni kama walivyotuacha wazee hao. Hakika leo tarehe 27 Aprili 2020 siyo siku ya furaha kwetu hata tuliokufahamu bali siku ya huzuni kubwa.

Amaa kweli duniani tunapita tu. Buriani kaka Mkubwa Evod Herman Mmanda mpendwa wetu. Kwa mapenzi yake Mola tutakuja kuonana siku parapanda itakapolia.

Nimehuzunika sana kaka. Sifa, Shukrani na Utukufu namrejeshea Muumba wetu na kumwomba akupumzishe mahala pema peponi, Amina.

Moses J. Machali.
error: Content is protected !!