July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bunge ngumi mkononi

Wabunge wa UKAWA wakiwa wamesimama bungeni wakiwa maamuzi ya Spika

Spread the love

WAKATI watanzania hawajaanza kufaidika na gesi iliyogundulika mkoani Mtwara, rasilimali hiyo imeendelea kuibua mzozo na mgogoro mkubwa Bungeni kiasi cha Spika Anna Makinda kuamua kuahirisha tena ghafla kikao cha 42 cha Bunge leo. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Jana Spika aliahirisha kikao cha 41 cha Bunge, baada ya wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani inayoundwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kupinga Serikali kuleta miswada mitatu nyeti kwa hati ya dharura kwa madai kuwa wabunge hawajaisoma na wadau hawajapata muda zaidi wa kuijadili.

Miswada hiyo ambayo ni mwiba mchungu Bungeni ni pamoja na muswada wa  Sheria ya Petroli, Muswada wa Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa mwaka 2015 na Muswada wa Sheria yaUwazi na Uwajibikaji katika taasisi za uchimbaji Tanzania wa mwaka 2015.

Mvutano huo  ulianza baada ya Mbunge wa Singida Mashariki, (Chadema) Tundu Lissu  kuomba mwongozo wa Spika kupinga kuletwa Bungeni kwa kwa miswada hiyo.

Wakati Lissu akiwa amesimama kuomba mwongozo, Spika Makinda kana kwamba hakumuona, aliendelea kumruhusu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene aendelea kuisoma miswada hiyo, mmoja baada ya mwingine ili ianze kujadiliwa na kisha kupitishwa.

Wakati Waziri Simbachawene akiendelea kusoma miswada hiyo, wabunge wa Ukawa walianza kusimama mmoja baada ya mwingine na hatimaye wote kujikuta wamesimama, kumpinga Waziri Simbachawene kuendelea kuisoma miswada hiyo.

Wabunge wao, walipoona Spika Makinda hataki kumsikiliza Lissu, walianza kuzomea na kupiga kelele kutaka asiendelee, hali iliyosababisha wabunge wa CCM nao  wajibu mapigo kwa kuzomea.

Kelele hizo za CCM na Ukawa zilimfanya Waziri Simbachawene asiweze kusikika na hatimaye Spika Makinda alisimama na kuahirisha kikao hicho cha Bunge kwa muda usiojulikana.

Hata hivyo kabla Spika Makinda hajaondoka kwenye kiti chake, alitaja baadhi ya majina ya wabunge wa Ukawa kwamba ndio walikuwa vinara wavurugu hizo na kuiagiza Kamati ya Haki Maadili na Madaraka ya Bunge  kuchukua hatua dhidi ya wabunge hao.

Wabunge waliotajwa kuwa vinara wa vurugu hao  John Mnyika (Ubungo), Lissu (Singida Mashariki), Moses Machalli (Kasulu Mjini), Peter Msigwa (Iringa Mjini) na David Silinde(Mbozi Magharibi).

Wengine ni Rajab Mbarouk (Ole), Felix Mkosamali (Muhambwe), Joseph Selasini, (Rombo) na Pauline Gekul (Viti Maalum Chadema).

“Hatuwezi kuendelea na Bunge katika mazingira haya ya vurugu na majina ya wabunge walioongoza vurugu nayapeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge,” amesema Makinda.

Mbali ya kuielekeza Kamati hiyo kushughulikia nidhamu ya wabunge hao, Spika Makinda aliagiza Kamati ya Uongozi ya Bunge kukutana mara moja kujadili mzozo huo na kuupatia ufumbuzi.

Mara baada ya Spika Makinda kuondoka, wabunge wa pande zote mbili, yaani wale wa CCM na Ukawa, kila kundi lilikusanyika kupanga mikakati ya vikao vijavyo vya Bunge kuhusu hatma ya miswada hiyo.

Wabunge wa CCM waliongozwa na Katibu wao, Jenister Mhagama wakati ukawa walikuwa chini ya Lissu.

Mhagama ambaye ni Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), alisikika akitoa maagizo kwa wabunge wa CCM kuwa msimamo wa kujadili na kupitisha miswada hiyo upo pale pale, wakati Ukawa nao walipania kuendelea na msimamo wa kuikataa miswada hiyo kwa sasa.

Wabunge hao waliendelea kubaki ndani ya ukumbi wa Bunge kwa takribani dakika kumi, huku kila upande ukirusha vijembe kwa mwingine kiasi cha kugeuza Bunge kuwa ukumbi wa mipasho.

Kabla ya timbwili hilo kuibuka Bungeni, Mbunge wa Ubungo mara baada ya kipindi cha maswali na majibu, aliomba mwongozo wa Spika kutaka kujua sababu ya Serikali kung’ang’ania kuleta miswada hiyo kwa hati ya dharura wakati kuna mambo ya msingi yanayopaswa kuja Bungeni kwa dharura.

Mnyika alitaja jambo linalopaswa kuja kwa hati ya dharura kuwa ni suala la Uandikishaji wa Wapiga Kura katika Daftari la Jipya la mfumo wa  BVR ambalo kasi yake ya uandikishaji inaenda kwa kusuasua.

“Mheshimiwa Spika, sisi hatutaki miswada hiyo ije sasa kwa hati ya dharura wakati haijajadiliwa vya kutosha na wabunge hawajapata muda wa kuisoma, tunataka shughuli za Bunge leo ziahirishwe na Bunge lipate fursa ya kujadili kwa dharula tatizo la BVR, lakini miswada hiyo kwa sasa hatuitaki,hatuoni udharula wake,” amesema  Mnyika.

error: Content is protected !!