January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bunge Maalum lisipuuze maoni ya wananchi

Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wakiendelea na vikao vya bunge hilo

Spread the love

BUNGE Maalum la Katiba “limenyofoa” maoni ya wananchi na kuingiza ibara zenye maslahi ya wabunge wa chama cha CCM.

Wakiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Wanaharakati wa ngazi ya jamii na washiriki wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) linaloratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) limelitaka bunge hilo kuzingatia mapendekezo ya wananchi.

Wanaharakati hao wamesema rasimu inayopendekezwa na bunge maalum imewanyima wananchi haki yao ya msingi ya kumwajibisha kiongozi (Mbunge au diwani) waliyemchagua kwa kura halali pindi anaposhindwa kutekeleza majukumu na ahadi alizozitoa wakati wa kampeni kwa wananchi.

Lakini rasimu ya bunge hilo imelipa uwezo bunge la Jamhuri ya Muungano kumuwajibisha Rais pindi akishindwa kutekeleza majukumu yake na akienda kinyume cha sheria na taratibu za nchi.

[pullquote]“Tunadai rasimu hii ya katiba iweke ukomo wa vipindi kwa wabunge kukaa madarakani. Iweke mfumo mzuri wa wananchi kuwawajibisha viongozi wasiotimiza majukumu yao kama ilivyo kwa bunge lilivyopewa dhamana na haki ya kumuwajibisha Rais anaposhindwa kutimiza wajibu wake,” amesema Esther Wiliam kwa niaba ya wa wanaharakati hao.[/pullquote]

Akizungumzia kuhusu mapungufu ya Ibara ya 111 kifungu cha (1) (d) Esther amesema kifungu hicho kimetaja sifa ya kuwa waziri au naibu waziri, kuwa ni lazima awe ni mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema “kifungu hicho kinaendeleza mgongano wa madaraka kati ya mihili mikuu miwili ya dola (Bunge na Serikali) kwa kumpa madaraka mbunge kuwa waziri au naibu waziri. Tunadai mawaziri wasiwe miongoni mwa wabunge ili kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa mihimili yote mitatu kwa kila mhimili kujitegemea”

Aidha, wanaharakati hao wameshangaa kuona katika ibara ya 22(2) (b) rasimu inayopendekezwa na bunge maalum ikitoa fursa ya bila ya ukomo kwa wawekezaji kuweza kutumia ardhi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na makaazi.

“Tunashauri kipengele hiki kiweke ukomo kwa wawekezaji kutumia ardhi ili kuweza kuepusha migongano na migogoro ya kimaslahi na ya kikatiba kati ya wananchi na wawekezaji katika suala zima la umiliki wa ardhi,” amesema Esther.

Esther ameitaja Ibara ya 257 kifungu cha (3) ni eneo lingine lenye mapungufu. Amesema kifungu hicho kimetoa uhuru kwa Benki kuu ya Tanzania (BOT) kutekeleza majukumu yake bila ya kuingiliwa, kudhibitiwa au kupewa maelekezo na mtu au mamlaka yoyote.

Kifungu hiki kinakinzana na dhana bora ya uwajibikaji na utawala bora na kinatoa mwanya wa ubadhirifu na matumizi ya mabaya ya fedha za umma kwa kigezo cha watendaji wa benki kuu kutowajibishwa kutokana na makosa yao kiutendaji pindi wanapokua madarakani. Kifungu hiki kinachochea na kutoa fursa ya ulimbikizaji kiporaji wa rasilimali na fedha za umma.

Masuala mengine ambayo yamepuuzwa na bunge hilo ni suala la maji kutotambuliwa kama haki ya msingi ya kikatiba na rasimu hiyo kutotamka wazi uwiano wa asilimia 50 kwa 50 kati ya wanawake na wanaume katika ngazi na nafasi mbali mbali za maamuzi.

error: Content is protected !!