JOB Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri amewaeleza wabunge wa bunge hilo kwamba, kesho Alhamis tarehe 22 Aprili 2021, kutakuwa na ugeni mzito. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Amesema, Rais Samia Suluhu Hassan atahutubia Bunge kama ilivyoelezwa awali na kwamba, si vizuri wabunge wakiwemo mawaziri na manaibu waziri kutokuwepo bungeni.
Akisisitiza uwepo wa wabunge wote, Spika Ndugai ameshauri wabunge wawaangalie wabunge wenzao na kama hawapo, wawapigie simu wasafiri usiku kwenda Dodoma.
“Kesho tutakuwa na ugeni mkubwa sana, Rais wa Awamu ya Sita anakuja kulihutubia Bunge. Huwezi kujua kesho wala kesho kutwa, si vizuri kutokuwepo kwenye Landmark ya mheshimiwa Rais wa awamu wa sita anapokuja kulihutubia Bunge hili,” amesema Spika Ndugai huku akisitiza, haipendezi gallery kujaa halafu ukumbi wa bunge kuwa wazi.
Rais Samia ambaye ni Rais wa Sita wa Tanzania, aliapishwa tarehe 19 Machi 2021 kuwa rais ikiwa ni siku mbili baada ya kutangazwa kifo cha mtangulizi wake, Hayati John Magufuli.
Rais Samia kesho tarehe 22 Aprili 2021, atalihutubia Bunge kwa mara ya kwanza tangu aapishwe kuwa kiongozi mkuu wa nchi.
Leave a comment