December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bunge lavunjika

Wabunge wa UKAWA wakitoka bungeni

Spread the love

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amelazimika kuahirisha Bunge baada ya mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kudai kuwa kumeingizwa bungeni, miswada mitatu mipya, kabla muswada wa kulinda watoa taarifa za uhalifu na mashahidi kuhitimishwa. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Mnyika alimtaka Spika Makinda, kuondoa miswada hiyo na ratiba ya Bunge ikarekebishwe; kauli ambayo ilionekana kumkera spika.

Alisema, ni jambo la kushangaza na la aibu kubwa kuona Spika Makinda, anaruhusu miswada hiyo mitatu ambayo ni muhimu kwa nchi, kuletwa kwa hati ya dharura bungeni.

Mnyika alieleza hayo kwa baada ya kuomba mwongozo kwa spika, ambapo alitumia kifungu cha 53, kifungu 1(6) cha kanuni za Bunge, kuwasilisha hoja yake.

Alisema, miswada iliyowasilishwa bungeni, tayari ilikataliwa na wabunge, tarehe 29 Juni wakati walipokuwa katika semina. 

Makinda alisema, hakuna mtu wa kumwamrisha ndani ya Bunge ili afanye kile ambacho mbunge anataka. Akamtaka Mnyika afute kauli yake ya kumtaka spika aondoe ratiba ya orodha ya shughuli za Bunge na kufuta kauli ya kutoa amri kwa spika. 

Baada ya Mnyika kuteleza agizo hilo ambalo pia lilipingwa na spika kwa madai kwamba hakuna kanuni iliyovujwa, ndipo wabunge wa upinzani walilisimama huku wakiimba nyimbo za kuibeza serikali.

Hata hivyo, wabunge hao walisema hawatoki ndani ya ukumbi wa bunge na ni zamu ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuondoka bungeni na kuwaacha wao.

Miswada ambayo iligomewa na wapinzani, ni muswada wa Sheria ya Kulinda watoa taarifa za uharifu; muswada wa sheria ya Petroli; muswada wa sheria ya usimamizi wa mapitio ya mafuta na gesi na muswada wa Sheria ya uwazi na uwajibikaji katika tasinia ya uchimbaji wa mwaka 2015.

Kwa pamoja, wabunge kutoka kambi rasim ya upinzani bungeni, walisimama kidete kugomea miswada hiyo mitatu ambayo iliwasilishwa katika orodha ya shughuli za bunge.

Wabunge hao walilazimika kusimama hadi Spika Makinda alipohailisha Bunge kwa kile ambacho wameita, “kuchoshwa kuburuzwa na kiti na serikali.” 

Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu, baada ya kuharishwa kwa Bunge alisema, kitendo cha serikali ya CCM kupeleka miswada minne bungeni kwa wakati mmoja ni uvunjifu wa kanuni za Bunge. 

Akizungumza na wabunge wa upinzani muda mfupi baada ya wabunge wote wa CCM kutoka nje, Lissu alisisitiza kuwa  kitendo cha miswada yote minne bungeni kupelekwa kwa wakati mmoja, ni ukiukaji wa kanuni za Bunge.

Bila kutafuna maneno, mbunge huyo machachari wa Singida Mashariki alisema, kitendo cha serikali kutaka kupitisha miswada hiyo haraka tena kwa hati ya dharula, ni shinikizo kutoka nje ili waweze kuwapatia fedha Desemba mwaka huu. 

Alisema, “Ndugu zangu nataka niwaambie kabla ya semina iliyofanyika juzi na wabunge wote kukataa upitishwaji wa miswada hii, tulikaa na maofisa wa wizara ya nishati na madini. 

“Wakatuambia ni lazima kuwepo kwa sheria za mikataba hiyo na wao watakuwa na kikao cha MCC Desemba mwaka huu na lengo kubwa ni kutaka kuipatia serikali fedha hivyo kama sheria hazitakuwa zimepitishwa serikali haitapata fedha.”

Alisema haiwezekani miswada minne ikapitishwa kwa wakati mmoja na mbaya zaidi miswada hiyo ikaingizwa bungeni kwa wakati mmoja tena kwa hati ya dharura.

Alihoji: “Kuna nini hadi serikali iwe na uharaka kiasi hicho?”

Akizungumzia umuhimu wa miswada hiyo alisema muswada pekee wa mafuta na gesi una vifungu 261 na vifungu vidogo zaidi ya 3000.

“Kwa hali hiyo ni nani mbunge ambaye anaweza kusoma vifungu hivyo tena ni vya kisheria, kwa siku moja? Mimi kama mwanasheria tena siyo mwanasheria wa kubabiasha, ninahitaji kupata miezi mitatu ili niweze kuuchambua vizuri, lakini kwa mwezi mmoja ninaweza kujua kuna vifungu vingapi kuna kurasa ngapi na wala siwezi kukuambia ndani ya sheria hizo kuna vitu gani,” alieleza Lissu.

Alisema kitendo wanachotaka kukifanya serikali hakina tofauti na kile ambacho Bunge lilifanya mwaka 1997 ambapo ilipitishwa sheria ya madini tena kwa hati ya dharula jambo ambalo lilisababisha taifa  kuwa na dhahabu lakini siyo mali yetu.

Alisema kwa mwaka huo huo ilipotishwa sheria ya wawekezaji ya kufuta kodi zote jambo ambalo linaendelea kulitafuta taifa. 

Kutokana na hali hiyo, Lissu alisema, kambi rasmi bungeni haiwezi kuona serikali inaendelea kupitisha miswada ambayo inakuwa sheria huku wananchi wakiendelea kutabika pasipokuwa na sababu.

Hata hivyo, alisema mara nyingi serikali imekuwa ikikataa kupitishwa miswada wakati wa bunge la bajeti. 

Alisema, “…imekuwa ni kawaida miaka yote kukataa kupitisha miswada katika kipindi kama hili, lakini cha kushangaza ni pale ambapo kwa bunge hili la bajeti serikali imekubali kupitisha miswada takribani 10 tena yote ni ya hati ya dharura.

Alisema, “Kwa uhai wa bunge, bunge hili linafanya kazi tofauti na mabunge yote yaliyopita ni sawa na bunge la kikoloni kwa maana sasa linaendeshwa kwa kuwaburuza wananchi.”

Mvutano huu umetokea, siku mbili baada ya Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene kuzomewa na wabunge kutokana na kutaka miswada hiyo ijadiliwe bungeni. 

Aidha, mbali na Simbachawene kuzomewa, Naibu wa waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage, nusura amrushie makonde mbunge wa Igunga, Dk. Dalaly Kafumu baada ya kupinga mswada huo kwa madai hauna tofauti na sheria za Uganda. 

Dk. Kafumu alisema, muswada uliyowasilishwa bungeni ni “Copy and Peste, isipokuwa limeondolewa neno Uganda tu.”

Wiki iliyopita, Bunge lilielezwa muswada wa sheria ya usimamizi wa mapato ya mafuta na gesi, una lenga kuhakikisha mapato yatokanayo na tasnia ya mafuta na gesi yanakusanywa na kutumiwa katika namna ambayo haihatarishi uimara wa kiuchumi wa nchi.

Akiwa mchangiaji wa kwanza, Lissu alisema, ni bora wabunge wote wakarejea katika historia ya nchi kwa kupitisha miswada miwili kwa hati ya dharura mwaka 1997 ambayo kwa sasa inawaumiza wananchi.

Alisema, ni jambo la kusikitisha kuona muswada huo unaweka kifungu ambacho kinazuia kuhoji mikataba ya zamani.

Kwa upande wake, Andrew Chenge, mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), alisema miswada hiyo inahitaji muda ili iweze kujadiliwa kwa kina. 

Chenge ambaye aliwahi kuwa mwanasheria mkuu wa serikali alisema, kupitisha miswada hii kwa haraka, hakutaisaidia serikali wala taifa. 

Chenge alisema wataalamu wanawajibu kutoa taarifa kuhusu ni mapungufu yapi kwa sheria ya awali ya miaka 1980 na sio kukimbilia kuja na miswada mipya ambayo inaonekana kuwa haikidhi mahitaji.

error: Content is protected !!