MASHIRIKA Yasiyo ya Kiserikali (NGO’S), 16 yakiongozwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), wameliomba Bunge lichukue hatua ili kulinda haki za wafugaji waishio karibu na hifadhi za taifa, ambao wanadaiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kuporwa mifugo yao na baadhi ya maafisa uhifadhi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Wito huo umetolewa leo tarehe 8 Novemba 2023 na Mkuu wa Idara ya Utetezi kwa Watetezi wa Haki za Binadamu THRDC, Paul Kisabo, akisoma tamko la mashirika hayo, jijini Dar es Salaam.
“Ni wakati sasa Bunge letu lichukue hatua sababu wabunge wamekuwa wakilalamika bungeni lakini hakuna mafanikio hivyo Bunge lihakikishe linalinda maslahi ya wananchi ambao linawawakilisha,” amesema Kisabo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Bob Chacha Wangwe, amesema ni ajabu kuona kwamba amri zinazotolewa na mahakama zenye lengo la kusuluhisha migogoro kati ya wafugaji na hifadhi kutotekelezwa na Serikali.
“Ni jambo la kushangaza kwamba serikali inakuwa haiheshimu maamuzi yaliyotolewa na mahakama kuhusu utatuzi wa baadhi ya migogoro ya wafugaji na hifadhi. Inabidi Serikali itekelze maamuzi na amri zilizowahi kutolewa na mahakama kuhusu migogoro hiyo,” amesema Wangwe.
Awali, Kisabo aliitaka Serikali iingilie kati sakata la baadhi ya wafugaji katika Hifadhi ya Ngorongoro ambayo inadaiwa ng’ombe zao 1,000 zinadaiwa kupigwa mnada kinyume cha sheria, ili warudishiwe mifugo yao.
Kisabo aliitaka Mamlaka ya Hifadhi za Tanzania (TANAPA), iache kusumbua wananchi wa Ngorongoro ili kutekeleza amri ya mahakama iliyoelekeza wananchi hao wasiondolewe hifadhini hadi kesi ya msingi waliyofungua kupinga hatua ya Serikali kutenga baadhi ya ardhi zao kuwa pori la akiba.
Madai ya wafugaji kunyanyaswa yamekuwa yakitolewa mara kwa mara, lakini TANAPA imekuwa ikikanusha kwa madai kuwa mifugo inayochukuliwa ni ile iliyoingia hifadhini kinyume cha sheria.
Leave a comment