September 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bunge lapitisha muswada sheria za fedha

Waziri wa Fedha na Mpango wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba

Spread the love

BUNGE la Tanzania limepitisha muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali za fedha wa 2022, wenye lengo la kurekebisha sheria zinazosimamia kodi na mrabaha, kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji viwandani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Muswada huo wa marekebisho ya sheria tano za fedha, umepitishwa leo Alhamisi, tarehe 22 Septemba 2022, baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, kuusoma kwa mara ya pili bungeni jijini Dodoma.

“Lengo la Muswada huu ni kufanya marekebisho kwenye Sheria zinazosimamia kodi na mrabaha, kwa kubadili viwango vya kodi na mrabaha na kuweka taratibu za utoaji vivutio kwa wawekezaji, ili kuhamasisha uzalishaji kwa viwanda vya ndani ya nchi vinavyozalisha mbolea na maguni ya mkonge, pamoja na kuondoa changamoto zilizopo hivi sasa katika utekelezaji wa Sheria ya uwekezaji Tanzania,” amesema Dk. Mwigulu.

Sheria zilizofanyiwa marekebisho ni pamoja na , Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147, ambapo kifungu cha 128 kimerekebishwa ili kumpa mamlaka waziri wa fedha, ya kusamehe ushuru kwenye bidhaa zitakazotumika katika utekelezaji wa miradi ya uwekezaji mahiri na mahiri maalum, itakayoidhinishwa na Kamati ya Taifa ya Uwekezaji (NISC).

Mwigulu amesema sheria hiyo imefanyiwa marekebisho ili kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye mvinyo unaotokana na zao la zabibu unaoingizwa ndani kutoka nje ya nchi, kutoka Sh. 2,466.45 kwa lita moja hadi Sh. 5,600 kwa lita.

Sheria nyingine iliyorekebishwa ni Sheria ya Kodi ya Mapato, sura ya 332, katika kifungu cha 10 ili kujumusiha uwekezaji mahiri ulioshinishwa na NISC, katika wigo wa maeneo ambayo waziri wa fedha anaweza kutoa msamaha wa kodi ya mapato.

“Hata hivyo, marekebisho yamefanyika katika Muswada ili kubainisha kwamba, Serikali itafuta msamaha husika pindi itakapojiridhisha kwamba msamaha husika haukutumia kama ilivyokusudiwa,” amesema Dk. Mwigulu.

Sheria nyingine iliyorekebishwa ni Sheria ya Madini, sura ya 123 ili kupunguza kiwango cha marabaha kwa malighafi za mbolea zinazochimbwa nchini, Phosphates Ore na Limestone, kutoka asilimia tatu hadi moja, kwa lengo la kutoa unafuu wa gharama za malighafi kwa wazalishaji wa ndani wa mbolea.

“Serikali ina imani kwamba, unafuu huu unaotolewa kwa wazalishaji wa mbolea utaleta matokeo chanya kwenye upunguaji wa bei ya mbolea kwa wakulima, na hivyo kupunguza mzigo kwa Serikali katika utoaji fedha za ruzuku kwenye mbolea,” amesema Dk. Mwigulu.

Mwigulu amesema sheria nyingine iliyorekebishwa ni Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, sura ya 148, ambapo imeongezwa kifungu kipya cha 55A, kwa kutoza kodi ya ongezeko la thamani kwa kiwango cha 0, katika mbolea inayozalishwa ndani ya nchi, kwa ajili ya kuwapa unafuu wakulima na watumiaji wa mbolea, kwa kupunguza gharama za uzalishaji wake viuwandani.

Akiendelea kusoma marekebisho hayo, Dk. Mwigulu amesema sheria hiyo ya ongezeko la kodi ya thamani, imerekebishwa ili kusamehe kodi hiyo kwa magunia ya mkonge yanayotengenezwa nchini.

“Vile vile, kufuatia majadiliano ya kina baina ya Serikali na Kamati ya Bunge ya Bajeti, inapendekezwa kupitia Jedwali la Marekebisho, kuondoa 6 pendekezo la kutoa msamaha kwa malighafi ya kutengeneza mitungi ya gesi inayotambulika chini ya HS Code 7229.90.00 na kutoa nafasi kwa Serikali kufanyia kazi zaidi pendekezo husika ili kujiridhisha kwamba malighafi husika haziwezi kutumika kwenye matumizi mengine na hivyo kupoteza mapato ya Serikali,” amesema Dk. Mwigulu.

error: Content is protected !!