August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bunge lanusa Ufisadi Nachingwea

Spread the love

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za serikali za Mitaa (LAAC) imenusa ufisadi katika Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, anaandika Dany Tibason.

Katika kikao cha kamati hiyo, kilichoketi mjini Dodoma chini ya Vedastus Ngombale, Mwenyekiti wa kamati hiyo, wajumbe wa kamati hiyo walishangazwa na halmashauri ya Nachingwea kudaiwa madeni mengi, huku ikishindwa kulipa fedha asilimia kumi kwa vijana na akina mama.

Abdalah Chikota, Makamu Mwenyekiti wa kamati ya LAAC alitaka kujua halmashauri hiyo, imepata wapi ujasili wa kutangaza taarifa ya ukaguzi wa fedha katika vyombo vya habari wakati baraza la madiwani halikukaa na kupitisha taarifa hiyo.

Ignas Malocha, Mbunge wa Kwela (CCM) amesema, asilimia 5 ambazo zilipaswa kulipwa kwa vikundi vya wamama ni Sh. 290 milioni huku zile za vikundi vya vijana zikiwa ni Sh. 299.4 milioni.

Naye Rose Kamili, Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA) alitaka kujua ni lini fedha hizo zitalipwa kwa makundi hayo kama sheria inavyoelekeza huku akihoji, kazi za maofisa maendeleo ya jamii na Idara ya Mashirika katika halmashauri hiyo.

“Hii inatupa picha juu ya uwepo wa ufisadi, halmashauri hii imeshindwa kabisa kuweka mikakati ya kimaendeleo wala kuweka wazi taarifa sahihi za kifedha,” amesema Kamili.

Mwenyekiti wa LAAC alipomtaka mkurugenzi kujibu hoja hizo, Bakari Mohamed Bakari, Mkurugenzi wa Nachingwea alijitetea kuwa hawezi kujibu jambo lolote kwani yeye ni mgeni katika halmshauri hiyo na wakati uteuzi unafanyika alikuwa nje ya nchi.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sitaweza kujibu jambo lolote lakini nitasaidiwa na watumishi wenzangu kwani mimekuja jana na wakati uteuzi wa wakurugenzi ukifanyika nilikuwa nje ya nchi na nimekuja hapa kutokana na umuhimu wa kikao hiki tu,” amejieleza.

Cecilia Kavishe, mtunza hazina wa halmashauri ya Nachingwea alipewa nafasi ya kutoa majibu ya maswali ya wajumbe wa LAAC, hata hivyo majibu yake hayakuwaridhisha wajumbe na hatimaye kutoa maagizo kwa halmashauri hiyo.

Vedastus Ngombale, Mwenyekiti wa kamati ya LAAC amesema kamati inaagiza halmashauri hiyo, kutorudia kutangaza taarifa za ukaguzi kabla ya Baraza la Madiwani kukaa.

Kamati hiyo pia imeiagiza halmashauri kutenga asilimia kumi ya mapato ya halmashauri kwa ajili ya mfuko wa vijana na akina mama kwani kwa kutofanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi.

Huku halmashauri hiyo ikitakiwa kuandika barua kwa kamati hiyo kabla ya 30 Agosti mwaka huu, barua hiyo iwe na ahadi ya kulipa madeni inayodaiwa ikiwemo asilimia kumi ya akina mama na vijana pamoja na ruzuku ya vijiji.

error: Content is protected !!