May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bunge laishauri Serikali imalizie viporo fedha za korosho

Bunge la Tanzania

Spread the love

 

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, imeishauri Serikali imalize kulipa madeni ya fedha za korosho, ilizonunua kwenye msimu wa 2018/2019. Anaripoti Nasra Bakari, DMC…(endelea).

Wito huo umetolewa na kamati hiyo, leo Jumatatu tarehe 24 Mei 2021, kupitia taarifa yake iliyowasilishwa bungeni na mjumbe wake, Khadija Aboud.

“Vilevile Kamati iliishauri Serikali kulipa fedha za korosho zilizonunuliwa na Serikali, kwa msimu wa Mwaka 2018/2019, kwa wakulima ambao walikuwa hawajalipwa. Ushauri huo haujatekelezwa,” imesema taarifa ya kamati hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo, Serikali haikulipa madeni hayo kwa maelezo kwamba, akaunti za benki za wakulima wanaodai, zilikuwa hazijatumika kwa muda mrefu.

“Ushauri huo haujatekelezwa kwa maelezo kwamba, wakulima hao hawajalipwa kwa sababu akaunti namba za benki walizowasilisha, zilikuwa hazijatumika muda mrefu (Dormant Account),” imesema kamati hiyo.

Zao la Korosho

Kamati hiyo imesema sababu zilizofanya wakulima hao wasilipwe fedha zao, hazina msingi.

“Kamati inaamini sababu hii haina msingi wowote, kwani benki zinao utaratibu wa kuhuisha akaunti ambazo hazijatumika muda mrefu (Activate Dormant Accounts),” imesema taarifa ya kamati hiyo.

Serikali ya Tanzania, chini ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli, iliamua kununua korosho za msimu huo, baada ya kuibuka mvutano baina ya wakulima wa korosho na wafanyabaishara, uliosababishwa na malalamiko ya bei ndogo.

Magufuli aliagiza Serikali yake inunue korosho hizo kuanzia Sh. 3,000 kwa kilo. Na kwamba, Serikali hiyo kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), ilinunua na kulipa kwa awamu.

Korosho hizo zilianza kununuliwa Novemba 2018 hadi 2019, ambapo Serikali ilinunua tani 214,269, zenye thamani zaidi ya Sh. 707 bilioni.

error: Content is protected !!