Spread the love

 

MFULULIZO wa matukio ya ajali za moto katika masoko mbalimbali nchini yamewaamsha wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitaka Serikali kulipa fidia kwa wafanyabiashara waliopoteza mali zao kutokana na ajali hizo.

Pia wameitaka serikali kuongeza magari ya zima moto ili kuwa na vifaa vya kutosha vitakavyowawezesha kukabiliana na matukio hayo. Anaripoti Rhoda Kanuti, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yameelezwa bungeni leo tarehe 10 Mei, 2022 na Mbunge wa Viti Maalumu, Cecili Paresso ambaye katika swali la msingi amehoji nini kauli ya Serikali juu ya matukio ya moto katika nasoko nchini.

Aidha, katika swali la nyongeza amehoji kwanini Serikali isiwalipe fidia wananchi walioharibiwa bidhaa zao kutokana na ajali hizo hasa ikizingatiwa Serikali inakusanya kodi na tozo mbalimbali kwao.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini amesema kuhusu suala la fidia ni suala la kisheria na hadi sasa hamna sheria inayoilazimu Serikali kulipa fidia kwenye matukio ya ajali za moto.

Akizungumzia matukio hayo ya moto, Sagini amesema uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vingine umebaini sababu mbalimbali za matukio hayo.

Ametaja sababu hizo ni pamoja na uunganishwaji holela wa mifumo ya umeme, kutokuzingatia tahadhari za moto kwa mama lishe na baba lishe na shughuli za uchomeleaji holela wa vyuma katika masoko.

“Katika kukabiliana na vyanzo vya matukio hayo umefanyika ukaguzi wa kinga na tahadhari ya majanga ya moto sambamba na utoaji wa elimu na mafunzo ya matumizi ya vifaa vya awali vya kuzima moto katika masoko nchini,” amesema.

Aidha, amesema Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji inashirikiana na Halmashauri zote kuboresha miundombinu ya kuzima moto katika masoko na kuhakikisha ramani za masoko mapya zinakaguliwa na zinakidhi vigezo vya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto.

Amesema serikali inaendelea kusisitiza uwepo wa vifaa vya awali vya uzimaji moto, uwepo wa ulinzi wa masoko kwa masaa 24 na kuzingatia utekelezaji wa mapendekezo ya taarifa maalum za kaguzi zinazotolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Aidha, baada ya majibu hayo, Mbunge wa Viti Maalumu, Zuwena Bushiri (CCM) naye amehoji ni lini serikali itapeleka magari ya kuzima moto katika manispaa ya Moshi kwani yaliyopo sasa ni ya taasisi ya TPC.

Akijibu swali hilo la nyiongeza, Sagini amesema katika bajeti ijayo Serikali itatenga fedha za kununua magari ambayo yatasambazwa katika maeneo yenye upungufu mkubwa wa vifaa hivyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *