May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bunge lahofia ukame, Spika atoa agizo

Bunge la Tanzania

Spread the love

 

KAMATI ya Kudumu ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira, limeonya uwezekano wa kutokea ukame nchini Tanzania, kufuatia kukithiri kwa vitendo vya ukataji miti. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Tahadhari hiyo, imetolewa leo Jumanne tarehe 27 Aprili 2021, bungeni jijini Dodoma na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Erick Shigongo wakati anawasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu uhifadhi na usimamizi wa mazingira.

Shigongo amesema, kwa mujibu wa taarifa ya Tatu ya Hali ya Mazingira ya Mwaka 2019, takribani hekta 469,420 za miti, hukatwa kila mwaka.

“Hali ya Mazingira nchini, iliyoripotiwa ndani ya taarifa hiyo inatia wasiwasi, imeripotiwa Tanzania bara inakisiwa kuwa na jumla ya hekari 48.1 milioni za misitu ambayo ni asilimia 51 ya eneo lote.”

“Lakini kuna ukataji holela wa miti unaokadiriwa takribani hekta 469,420 kwa mwaka,” amesema Shigongo

Mwenyekiti huyo amesema, “na tatizo hili linaendelea kukua kwa kasi mwaka hadi mwaka nchi nzima.”

Erick Shigongo Mbunge wa Buchosa (Ccm)

“Moja ya sababu inayopelekea kuwa na ukataji mkubwa wa miti nchini ni umasikini kwani asilimia kubwa ya watanzania wanategemea mazao ya misitu katika kutimiza mahitaji yao,” amesema

Baada ya Shigongo kutoa taarifa hiyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alimuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, apeleke bungeni taarifa ya hali ya mazingira nchini, kwa ajili ya kujadiliwa.

“Katika taarifa ya kamati wametukumbusha kwamba, kuna taarifa ya hali ya mazingira nchini ambayo huwa inatakiwa tuletewe bungeni periodically. Ni kwa muda mrefu sijaona taarifa hii ikiletwa,” amesema Spika Ndugai na kuongeza”

“Waziri hii ni home work mojawapo, uwaambie wataalamu wako taarifa yetu tunaitaka sasa, tunaidai sababu ni moja ya taarifa muhimu sana. Taarifa ya hali ya mazingira nchini inatuonyesha hali halisi itakavyokuwa.”

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

Kufuatia changamoto hiyo, Jafo amesema wizara yake imeandaa Mpango Kazi Mpya wa Taifa wa Hifadhi ya Mazingira wa Mwaka 2021-2026, ili kuondoa changamoto mpya za mazingira.

Jafo amesema mpango huo umeandaliwa baada ya wizara hiyo kupitia Mpango Kazi wa Taifa wa Hifadhi ya Mazingira wa Mwaka 2013-2018, uliomaliza muda wake.

“Lengo la mapitio hayo ni kuhuisha changamoto na masuala mapya ya mazingira yaliyobainishwa katika Taarifa ya Tatu ya Hali ya Mazingira ya mwaka 2019, Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo (2021 – 2026 na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2015 – 2030,” amesema Jafo.

Sambamba na hilo, Jafo amesema katika kipindi cha mwaka 2020/21, ofisi yake imepitia Mpango wa Taifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame ili kuhuisha changamoto za uharibifu wa ardhi.

Hata hivyo, Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) inatekeleza Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula Katika Maeneo Kame ya Tanzania – LDFS, wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 7.156.

Suleiman Jaffo, Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

“Na utatekelezwa katika kipindi cha 2017 hadi 2022. Mgawanyo wa fedha hizi ni Dola za Marekani milioni 5.706 kwa Tanzania Bara na Dola za Marekani milioni 1.45 kwa Zanzibar. Mradi una lengo la kuboresha mifumo ikolojia ya kilimo ambayo itawezesha kuongeza uzalishaji wa chakula,” amesema Jafo na kuongeza:

” na kuboresha mazingira na usimamizi endelevu wa mifumo ikolojia inayochangia kutoa huduma muhimu za uzalishaji kwenye maeneo ya ardhi, maji, misitu na bioanuai kwa madhumuni ya kuboresha uzalishaji.”

Maeneo yanayonufaika na utekelezaji wa mradi huo kuwa ni Dodoma,Tabora, Singida na Mwanza. Na kwa upande wa Zanzibar unatekelezwa katika wilaya ya Michweni na Kaskazini Pemba.

error: Content is protected !!