Monday , 11 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Bunge laahairishwa, maswali 123 yaulizwa
Habari za Siasa

Bunge laahairishwa, maswali 123 yaulizwa

Bunge la Tanzania
Spread the love

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limehailishwa hadi tarehe 6 Novemba, 2019, baada ya wabunge kufanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupitisha marekebisho mbalimbali ya Miswada ya Sheria. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Mbali na kupitisha marekebisho ya sheria wabunge walipata fursa ya kuuliza maswali ya msingi 123 na maswali sita ya papo kwa papo yaliulizwa na kujibiwa na Waziri Mkuu. 

Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu Kasim Majaliwa alipokuwa akihailisha bunge leo Bungeni jijini Dodoma.

“Wabunge walipata fursa ya kujadili na kupitisha Miswada minne iliyowasilishwa na Serikali katika Mkutano huu.

Miswada ya Sheria iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge katika mkutano huu ni Muswada wa Sheria ya Serikali Mtandao wa Mwaka 2019, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2019, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.5) wa Mwaka 2019 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.6) wa Mwaka 2019.

Majaliwa alisema kuwa bunge lilijadili na kuridhia maazimio nane kama vile, Azimio la Kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC na kuendesha vyema Mkutano wa 39 wa Jumuiya hiyo uliofanyika Dar es Salaam, Tanzania.

Maazimio mengine ni Kuridhia Mkataba wa Minamata Kuhusu Kupunguza kwa kadiri iwezekanavyo Matumizi ya Zebaki ifikapo Mwaka 2030 na Azimio la Kuridhia Itifaki ya pamoja ya ziada ya Nagoya Kuala Lumpur kuhusu Uwajibikaji Kisheria na Fidia kwa Madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa katika kutekeleza Itifaki ya Cartagena.

Mengine ni Azimio la Kuridhia Itifaki ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu Kulinda Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea, Azimio la kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Azimio la kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Kigosi kuwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi.

Pia Azimio la kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji wa Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Ugalla kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla na Azimio la Kuridhia Itifaki ya Marrakesh inayowezesha Upatikanaji wa Kazi zilizochapishwa kwa Watu Wasioona, Wenye Uoni Hafifu au Ulemavu Unaofanya Mtu Kushindwa Kusoma ya Mwaka 2013″aliainisha Majaliwa.

Majaliwa alisema Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika Kimataifa. “Ukweli wa hili unajidhihirisha katika matokeo ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

“Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo Kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) na juhudi za Serikali katika kujenga miundombinu wezeshi ya kiuchumi kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara na hivyo, kurahisisha utekelezaji wa dhana ya diplomasia ya uchumi,” alisema Majaliwa.

Majaliwa alisema miongoni mwa mafanikio ya Uenyekiti wa Tanzania kwenye Mkutano huo ni kitendo cha Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kupitisha matumizi ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini wa Afrika sambamba na lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kireno. Kwa kuanzia lugha ya Kiswahili itatumika katika mikutano ya Wakuu wa Nchi na Serikali na Baraza la Mawaziri.

Alisima Tanzania inaendelea kujivunia historia ya lugha ya Kiswahili hususan matumizi yake wakati wa harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika na pia kuwa miongoni mwa lugha rasmi za Umoja wa Afrika.

“Nitoe wito kwa wadau wote wa Kiswahili nchini, watumie vyema fursa hii kutengeneza ajira kupitia huduma za ukalimani, ufundishaji na masuala mengine yenye kuhusisha matumizi ya lugha hii adhimu yenye kuakisi utamaduni wa Mwafrika.

“Naiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kujipanga vizuri ili kuchangamkia fursa hiyo muhimu”alisema.

Majaliwa alisema ikumbukwe  kwamba Tanzania imeanza kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara chini (Blueprint on Regulatory Reforms For Improved Business Environment) na Mpango Kazi wa Utekelezaji wake tangu Julai mosi, 2019.

“Aidha, sote tunatambua kuwa lengo la blueprint ni kujenga mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji ambapo kupitia Mkutano wa 15 wa Bunge la 11 jumla ya kodi na tozo 54 ziliondolewa.

“Sambamba na hilo, Serikali imeunda Timu ya Wataalamu ambayo inafanya uchambuzi wa   changamoto zilizobainishwa kwenye taarifa mbalimbali na kuandaa mapendekezo ya marekebisho ya sheria husika. Aidha, kama nilivyoeleza katika hotuba yangu.

“Kwa upande mwingine, nitumie fursa hii kumpongeza tena Mheshimiwa Rais kwa hatua za makusudi anazochukua kuhakikisha anaimarisha shughuli za biashara na uwekezaji kupitia ziara za kitaifa za viongozi rafiki kutoka mataifa mbalimbali sambamba na makongamano ya kibiashara na uwekezaji.

“Kati ya Agosti na Septemba 2019, Mheshimiwa Matalema Cyril Ramaphosa, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini na Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda walifanya ziara rasmi za Kiserikali nchini Tanzania. Vilevile, ziara hizo muhimu ziliambatana na makongamano ya biashara na uwekezaji kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na nchi hizo” Alisema Majaliwa.

Majaliwa alisema kuwa hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini imeendelea kuwa toshelevu.

Alisema  kwa mfano, katika msimu wa kilimo wa 2018/19 uzalishaji ulifikia takriban tani 16.41 milioni ikilinganishwa na mahitaji ya tani 13.84 milioni.

Alisema kuwa hivi sasa wafanyabiashara wa mazao ya chakula wanaendelea kusafirisha na kuuza mazao hayo ndani na nje ya nchi.

“Serikali inawahimiza wananchi wote kuhifadhi chakula cha kutosha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani hususan wakati huu tunapoingia kwenye msimu mpya wa kilimo kwa mwaka 2019/20,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema katika maandalizi ya msimu mpya: “Katika  kipindi hiki cha kuanzia Septemba 2019 maeneo mengi ya nchi yetu huanza kupata mvua za vuli ambazo ni ishara ya kuanza kwa msimu mpya wa kilimo. Serikali inahakikisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu bora, mbolea na viuatilifu kwa ajili ya msimu huu mpya wa kilimo.

“Nitumie  nafasi hii kuiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe inasimamia ipasavyo mawakala waliopewa jukumu la kusambaza pembejeo kwa wakulima ili ziwafikie kwa wakati na kwa bei inayohimilika na ubora unaohitajika,” alisema Waziri Mkuu.

Akizungumzia zao la Pamba, Waziri Mkuu Majaliwa amesema mabadiliko ya bei ya pamba katika soko la dunia yamesababishwa na mgogoro wa kibiashara kati ya mataifa makubwa yameporomosha bei ya pamba katika soko la dunia kinyume na matarajio kuwa bei ingeongezeka.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua zifuatazo: “Kusimamia makubaliano kati ya Benki Kuu na Benki zilizotoa mikopo kwa kampuni zinazonunua pamba kulingana na mahitaji yao ya mitaji ya kununua pamba ili pamba yote inunuliwe kwa wakati;

“Kuhamasisha makampuni kupeleka fedha kwa ajili ya malipo ya wakulima na kulipia pamba iliyopimwa ghalani na iliyobaki mikononi mwa wakulima.

“Kudhibiti udanganyifu kupitia mizani, malipo ya wakulima na makato ya pembejeo katika maeneo yaliyobainika kutokea kwa vitendo hivyo.

“Hivi sasa, wanunuzi wote wamepewa maeneo yote yenye Pamba na tayari wameshapewa fedha kwa ajili ya kulipia Pamba yote.

“Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kusimamia manunuzi haya ili wakulima walipwe malipo yao stahiki”alisema Majaliwa.

Akizungumzo korosho katika msimu wa 2018/19 jumla ya tani 224,964 za korosho ghafi zenye thamani ya shilingi bilioni 729.90 zilikusanywa.

Alisema kuwa kati ya hizo, tani 222,825 zilikusanywa na Serikali, aidha, korosho zilizolipwa ni tani 197,547 na Serikali inakamilisha malipo ya kiasi kilichobaki cha tani 25,278.

Alisema kuwa hivi sasa, korosho yote imenunuliwa na inasafirishwa, aidha, baada ya zoezi hilo Bodi ya Mazao Mchanganyiko itarudi kulipa madeni yaliyobaki kwa wakulima na wenye maghala.

Alisema katika kuelekea msimu ujao wa ununuzi wa korosho, Serikali imeandaa mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika. Jitihada zinazofanywa na Serikali hivi sasa ni:-

“Kuvutia uwekezaji katika viwanda vya kubangua korosho nchini.

“Kupanua soko la korosho kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kutengeneza bidhaa nyingine zitokanazo na korosho zikiwemo siagi, maziwa, mvinyo na sharubati.

“Kuendelea kujenga maghala ya mfano na yenye viwango kwa ajili ya kuhifadhia korosho katika maeneo ya kimkakati;

“Kusimamia uuzwaji wa korosho inayozalishwa nchini kwa wakati ili kutumia fursa ya korosho ya Tanzania ambayo inazalishwa kipindi ambacho hakuna korosho nyingine katika soko la dunia.

“Kuimarisha mifumo ya ununuzi wa korosho kwa lengo la kuvutia wanunuzi wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi” alisema Majaliwa”alisema.

Kuhusiana na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Waziri Mkuu Majaliwa amesema tarehe 24 Novemba, 2019, nchi  itaingia kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano.

“Lengo la uchaguzi huo ni kukidhi matakwa ya Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, inayoelekeza kuwa Mamlaka na Madaraka ya Serikali yanatokana na wananchi”alisema Majaliwa.

Majaliwa alisema kuwa wakati wa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa anapenda kusisitiza mambo kadhaa ambayo ni .

“Kuwasihi Waheshimiwa Wabunge na Madiwani kuhamasisha wananchi kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa. Natoa rai kwenu kuhakikisha mnashiriki kikamilifu katika shughuli zote za uchaguzi huo;

“Kuwahimiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuratibu shughuli za uchaguzi katika maeneo yao na kuhakikisha uwepo wa ulinzi na usalama wakati wote wa uchaguzi hasa kipindi cha Kampeni na wakati wa kupiga kura.

“Vyombo vya ulinzi na usalama vishiriki kikamilifu kuhakikisha wananchi wanafanya uchaguzi katika mazingira ya amani na utulivu bila kubughudhiwa; na

“Kuwahimiza Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kuhakikisha wanazielewa Kanuni na miongozo ilitoyotolewa ili waweze kutoa tafsiri sahihi wakati wa kusimamia uchaguzi huo na kuhakikisha unafanyika kwa ufanisi mkubwa kwa mujibu wa Sheria.

“Naomba kutoa wito kwa Watanzania wote wenye sifa kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura, kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali na kushiriki kupiga kura kwani hiyo ni haki yao ya kikatiba kwa kuzingatia misingi ya demokrasia.

“Naomba nitoe rai kwa wadau mbalimbali watakaoshiriki katika uchaguzi wakiwemo Vyama vya Siasa, Taasisi za Serikali na Zisizo za Serikali na Wananchi kusoma na kuzielewa Kanuni na miongozo ya uchaguzi kwa kuhakikisha wanajiepusha na vitendo vyovyote vya rushwa na uvunjifu wa amani.

“Serikali haitasita kuchukua hatua pale itakapothibitika vitendo hivyo kufanyika kinyume cha Kanuni na Sheria nyingine za nchi”alisema Majaliwa

Kwa upande wa uboreshaji wa daftari la wapiga kura, tarehe 18 Julai, 2019 Serikali ilizindua zoezi hilo mkoani Kilimanjaro.

Alisema kuwa Uboreshaji huo, unahusisha Wapiga Kura waliotimiza umri wa miaka 18 na wale watakaotimiza umri huo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Alisema kuwa makundi mengine yatakayohusika ni wapiga kura waliohamia katika kata au jimbo jingine la uchaguzi, waliopoteza kadi au kuharibika, wanaohitaji kurekebisha taarifa zao.

Alisema mfano majina ambayo hapo awali yalikuwa yamekosewa pamoja na kuwaondoa wapiga kura waliopoteza sifa kama vile kufariki.

Alisema kuwa kwa sasa zoezi hilo tayari limekamilika katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Mara na Mwanza (isipokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba).

Zoezi hilo linaendelea kutekelezwa chini kwa kaulimbiu isemayo Kadi Yako, Kura Yako, Nenda Kajiandikishe.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Jaji Kiongozi akerwa wananchi kukosa imani na mahakama

Spread the loveWATENDAJI wa Mahakama ya Tanzania, wametakiwa kuweka mikakati itakayosaidia kurejesha...

BurudikaHabari za Siasa

Samia amchangia Professa Jay mil. 50, Chadema, wasanii wamwaga manoti

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amechangia kiasi cha Sh 50 milioni...

Habari za Siasa

Biteko: Samia ni muumini wa maridhiano sio kwa kuigiza

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Mpango: Sitakufa bali nitaishi

Spread the loveMAKAMU  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk....

error: Content is protected !!