July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bunge lacharuka mikopo makundi maalumu isipunguzwe

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson

Spread the love

 

WABUNGE wameiomba Serikali isipunguze kiwango cha mikopo inayotolewa na halmashauri kupitia mapato ya ndani kwa watu wa makundi maalum. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Ombi hilo limekuja baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba kupendekeza mgao mpya wa asilimia 10 ya mapato hayo vyanzo vya ndani vya halmashauri kwamba asilimia tano iwe kwa ajili ya miundombinu na masoko ya machinga.

Asilimia mbili kwa vijana, asilimia mbili kwa wanawake na asilimia moja kwa watu wenye ulemavu.

Hata hivyo, leo tarehe 20 Juni, 2022 wakichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2022/23, bungeni jijini Dodoma, baadhi ya wabunge wamepinga mgao huo.

Mbunge wa Viti Maalum, Dk. Christine Ishengoma (CCM), amesema mikopo hiyo ilipaswa kuongezeka badala ya kupunguzwa kutoka asilimia 10 iliyokuwepo hadi kufikia asilimia tano.

“Hii asilimia 10 umesema asilimia mbili itakwenda kwa vijana, moja itakwenda kwa watu wenye ulemavu, kwa kweli hapo haileweki. Ninachoomba hii asilimia 10 ibaki kama ilivyokuwa asilimia nne ibaki kwa kina mama, nne kwa vijana na mbili ibaki kwa wale wenye ulemavu.

“Kile kilichokuwa kinaombwa ni kuongeza bajeti kwa upande wa asilimia 10, badala ya kuongezwa inapunguzwa. Naomba waziri aangalie vizuri sana kusudi isipangwe kama anavyokusudia iende,” amesema.

Dk. Ishengoma amekosoa hatua ya asilimia tano zilizopunguzwa kwenda kwa kundi la wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga, akisema wametengewa fedha katika maeneo mengine.

“Ningependa kuongezela asilimia 10, kwa kweli hii asilimia ukija kuhitimisha naomba uitolee ufafanuzi tuweze kuelewa. Umesema asilimia tano imependekezwa kuwa iende kwa wamachinga, kusudi kuboresha miundombinu ya ujenzi na masoko. Ukiangalia wamachinga kuna fedha zimeshatengwa,” amesema Dk. Ishengoma.

Awali Mbunge wa Viti Maalumu Tanga, Husna Juma Sekiboko amesema chanzo hicho cha mikopo kilichoanzishwa mwaka 1993, maboresho ya 2018 na 2019, hakitoshi.

Amesema fedha inayotolewa kama mikopo haitoshi kwani kuna halmashauri nyingi zinakusanya chini ya Sh bilioni moja.

“Haifiki hata asilimia 10 kiujumla haifiki hata Sh milioni 200 hivyo Halmashauri inaishia kuwakopesha Sh milioni moja au mbili ambazo ni ndogo sana,” amesema.

Aidha, Mbunge wa Vitimaalum, Shali Raymond naye amesema mwaka 2008 Serikali ilitoa mgawo mpya ambapo badala ya asilimia 10, ikawa asilimia nne kwa akina mama, asilimia nne kwa vijana na mbili walemavu.

“Mheshimiwa Waziri ni Mbunge anajua jambo linaloendelea hela nyingine ilibidi wa hela wabunge wasaidie vikundi hivi kutoka mfukoni mwao.

“Sasa unagusa tena palepale yaani unaweka chumvi kwenye kidonda. Kwani wanawake wakipata si jamii imepata? Naomba sana waachieni wanawake hiyo asilimia yao tano kama ilivyokuwa,” amesema.

error: Content is protected !!