BUNGE la Tanzania, limeiagiza Serikali, ifanye uchunguzi wa mifumo inayoratibu shughuli za kitabibu na hesabu za Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Agizo hilo limetolewa leo Alhamisi, tarehe 10 Juni 2021, bungeni jijini Dodoma na Spika wa Bunge, Job Ndugai, akisoma mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kuhusu mashirika yaliyoshindwa kuwasilisha kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), taarifa za hesabu kwa mwaka 2019/2020, kwa ajili ya ukaguzi.
Bunge limeagiza uchunguzi huo, baada ya MOI kushindwa kukamilisha hesabu zake kwa mwaka huo wa fedha, kufuatia taarifa za mifumo hiyo kutolingana.

Kufuatia changamoto hiyo, Spika Ndugai amesema, bunge linaishauri Serikali ifanye uchunguzi wa mchakato mzima wa ununuzi na usimikaji wa mfumo wa shughuli za kitabibu, wa taasisi hiyo.
“Kuhusu MOI kutokukamilisha hesabu, kutokana na changamoto ya mfumo wa kitabibu kutowasiliana ipasavyo na mfumo wa hesabu. Tunashauri Serikali ifanye uchunguzi wa mchakato mzima wa ununuzi na usimikaji, mfumo wa shughuli za kitabibu uliopo MOI,” amesema Spika Ndugai.
Kiongozi huyo wa Bunge ameongeza “kubaini iwapo taratibu zilifuatwa na kama mfumo huo una manufaa kwa Taifa.”
Wakati huo huo, Spika Ndugai ameishauri Serikali ipeleke watalaamu wenye sifa katika taasisi hiyo, kwani MOI ina tatizo la ukosefu wa wahasibu wasio na vigezo.
“Aidha, Serikali ipeleke wataalamu wenye sifa MOI kutekeleza shughuli za ukaguzi na uhasibu. Tunapata shida ya wahasibu MOI kutokana na sifa zao, tupate ambao ni more qualify (wanaokidhi vigezo),” amesema Spika Ndugai.
Leave a comment