March 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bunduki zatumika kumkamata Lissu

Spread the love

ASKARI 17 wa Jeshi la Polisi wametumika kumkamata Tundu Lissu, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika TLS, eneo la Kisutu, Dar es Salaam, anaandika Hellen Sisya.

Miongoni mwa watu hao, 13 walionekana kuwa na silaha za moto, wakiwa ndani ya magari matatu, walisimamisha gari alimokuwamo Lissu nje ya geti la Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu saa 7.14.

Mmoja wa maofisa hao, akiwa amevaa nguo za raia, alifuata gari la Lissu na kuomba kufunguliwa dirisha, ndipo LIssu alipofungua na kuhoji- “nikusaidie nini?”

“Mimi ni ofisa wa usalama, tunakuhitaji Central Police (Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam),” alisikika ofisa huyo akijitambulisha.

“Mnataka nini na naitwa kwa ajili ya nini huko,” alihoji Lissu.

“Tunakuhitaji kwa ajili ya mahojiano,” alieleza ofisa huyo ambaye jina lake halikusikika vyema.

“Basi nakuja, tuongozane, mimi nakuja kwa gari langu,” alisema Lissu na kukataliwa na ofisa huyo, ambaye wakati akiendelea kuzungumza na Lissu, alisogea ofisa mwingine ambaye alisema lazima apande gari walilokuwamo wao. Gari hilo – Toyota Landcruiser, lilikuwa na namba za usajili – RX04 EZN.

Baada ya muda, Lissu alishuka ndani ya gari lake na kwenda kupanda gari la maofisa hao na kuanza safari ya kwenda kituo kikuu cha polisi, eneo la Stesheni.

Mbali na gari alilokuwamo Lissu, magari mengine mawili yaliyokuwa na polisi wenye silaha yalifuata “msafara” huo – Lissu akiwa mtuhumiwa wa makosa ambayo hayakutajwa.

Baadhi ya maofisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mawakili wa Lissu walipofika  kituo kikuu cha polisi, walizuiwa kuingia ndani ya jengo hilo na maofisa wa polisi.

“Haturuhusu mtu yeyote kutoka popote kuja kumuona Lissu, hapa hayupo na hata kama yupo, hamruhusiwi kufika hapa. Hii ni order (amri) kutoka juu, naomba muondoke,” alisema ofisa aliyekuwa lango la kuingilia kituoni hapo.

Awali, kuanzia asubuhi, Lissu alikuwa mahakamani hapo akiwa wakili katika kesi ya makosa ya kimtandao inayomkabili Yericko Nyerere.

error: Content is protected !!