August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bundi anyemelea kanisa la Anglikana,

Spread the love

HALI si shwari katika kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN), baada ya waumini wa kanisa hilo kudaiwa kumsusia ibada kanisani, Askofu Boniface Kwangu, Kiongozi mkuu wa dayosisi hiyo, anaandika Moses Mseti.

Askofu Boniface anatuhumiwa kutumia vibaya mali za kanisa hilo, kitendo ambacho kimewakera waumini wa kanisa hilo na hatimaye kuamua kuchukua uamuzi wa kuanza kususia ibada zinazoongozwa na askofu huyo.

Wakati waumini hao wakichukua uamuzi huo, baadhi yao wamesema kuwa, wanashangazwa na hatua ya polisi wa jiji hilo kuamua kuwalinda mwanzo-mwisho wakati wa ibada za wiki mbili zilizopita yaani Septemba 4 na Septemba 11, mwaka huu.

Mmoja kati ya waumini wa kanisa hilo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe na MwanaHALISI online, amesema “Suala la polisi kuja kanisani wakati wa ibada na kutulinda linatushangaza sana.”

Huku akiongeza kuwa, “Katika ibada za wiki mbili zilizopita ambapo Joseph Samuel, Mchungaji Msaidizi wa kanisa letu, aliongoza ibada, lakini Askofu Boniface akaingia kanisani akiwa na ulinzi wa polisi wawili wakaenda kukaa kwenye viti vya viongozi wa kanisa.”

Akizungumza kwa niaba ya waumini wenzake, muumini huyo amesema, mgogoro wao na Askofu huyo ambaye kwa muda mrefu alikuwa Marekani kwa mapumziko lipo makao makuu ya kanisa Dodoma na hata Askofu Mkuu analifahamu.

“Tumemgomea kutuongoza na wala kuendesha ibada kutokana na tuhuma alizonazo na kwa kuzingatia msingi ya kiimani. Waumini wengi tulitoka nje na kumuacha kiongozi huyo na baadhi ya viongozi wachache wanaomuunga mkono, wakaendelea na ibada.” Amesema.

MwanaHALISI online limezungumza na Joseph Samuel, Kiongozi Msaidizi wa kanisa hilo, ambapo amesema, “Ni kweli kabisa. Ndivyo ilivyo na hata CD inayoonyesha matukio hayo ipo ofisini kwetu.”

Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, alipoulizwa kuhusiana na polisi kuwalinda waumini wakati wa ibada, amesema “Viongozi wa kanisa walituomba wenyewe tuwalinde lakini nje ya kanisa wala si ndani. Walihofia kuwa kungetokea vurugu wakati wa ibada.”

Kamanda Msangi amesema zaidi kuwa, niliwataka vijana wangu wasimguse yeyote, labda pale watu watakapohatarisha usalama wa watu na mali.”

Alipotafutwa Askofu Boniface kupitia simu yake ya mkononi, alisema hawezi kutolea ufafanuzi suala hilo kwa wakati huu kwani yupo katika ziara ya huduma za kanisa mkoani Geita.

“Nipo kwenye huduma sasa hivi, kwanza ninapoendelea kuongea na wewe hapa nachelewa kufanya majukumu yangu, wambie hao waliokupa taarifa hizo ndiyo wakupe maelezo sahihi,” amesema Askofu Boniface Kwangu na kukata simu.

error: Content is protected !!