UPANDE wa utetezi kwenye kesi inayowakabili viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa mshtakiwa namba tisa amelazwa. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).
Mshtakiwa wa tisa ni Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini. Wengine ni Freman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa; Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu Chadema; John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara; Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.
Wengine ni Halima Mdee, Mbunge wa Kawe; Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini; Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini na John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini.
Leo tarehe 7 Oktoba 2019, mbele ya Hakimu Thomas Simba, Profesa Abdallah Safari ambaye ni wakili mwongoza jopo la utetezi akisaidiwa na Peter Kibatala na John Mallya, ameieleza mahakama kuwa Bulaya amelazwa katika Hospitali ya Agha Khani na kwamba mahakama imsikilize mdhamini wake kwa maelezo zaidi.
Ndeshukuru Tungaraza, mdhamini wa Bulaya ameieleza mahakama kuwa mdhamana wake anaumwa na amelazwa hospitali.
Prof. Safari ameiomba mahakama kuahirisha shauri hilo kwa kuwa, mshtakiwa mmoja hayupo kama yalivyo mataka ya sheria.
Faraja Nchimbi, Wakili wa Serikali Mkuu aliyeongoza jopo la mawakili wa serikali, anayesaidiana na Dk. Zainab Mango, wakili wa Serikali Mkuu; Wankyo Simon, Wakili wa Serikali Mwandamizi na Salim Msemo wakili wa Serikali.
Nchimbi amedai mahakamani hapo, kuwa kwa mujibu wa taarifa za mgonjwa (Bulaya), anatakaiwa kupumzika hadi tarehe 10 Oktoba 2019 ambapo siku ya pili yake tarehe 11, kesi itaendelea na kwamba shauri hilo lipangwe tarehe za karibuni.
Baada ya kusikiliza pande zote, Hakimu Simba ameahirisha shauri hilo mpaka tarehe 15, 17 na 18 Oktoba 2019 saa nne na nusu asubuhi.
Leave a comment