Monday , 11 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Bulaya ataka Balozi Sirro ahojiwe bungeni upotevu mabilioni fedha mfuko wa Polisi
Habari za Siasa

Bulaya ataka Balozi Sirro ahojiwe bungeni upotevu mabilioni fedha mfuko wa Polisi

Spread the love

MBUNGE wa Viti Maalum, Ester Bulaya, ametaka aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, apelekwe bungeni jijini Dodoma, kwa ajili ya kuhojiwa juu ya upotevu wa mabilioni ya fedha za Mfuko wa Tozo wa Kufa na Kuzikana wa Jeshi la Polisi, unaodaiwa kutokea wakati akiwa madarakani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Bulaya ametoa wito huo leo tarehe 3 Novemba 2023, bungeni jijini Dodoma, akichangia taarifa za kamati za kudumu za Bunge juu ya ripoti ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha ulioshia Juni 2022.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 66(3) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi, kimeainisha kuwa IGP ndiyo mwenye mamlaka ya matumizi ya fedha kwenye mfuko huo na 2018 mpaka 2021 IGP alikuwa Sirro. Mfuko huu umetajwa ufisadi wa Sh. 1 bilioni, anayeidhinisha fedha hizi alikuwa Simon Sirro,” amesema Bulaya.

Bulaya amesema “mleteni kokote aliko aje apambanane na hali yake, hamuwezi mkafumbia macho hivi vitu. Leo Sirro yuko wapi, si balozi? arudishwe aje abebe mzigo wake, hakuna Bunge la kulinda watu wa namna hii.”

Bulaya amesema upotevu wa fedha hizo unawaathiri askari polisi ambao wanakatwa mishahara yao kwa ajili ya kuzichanga ili ziwasaidie wanapopata matatizo.

Balozi Sirro alistaafu Jeshi la Polisi mwaka 2022, kisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alimteuwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, kisha nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camilius Wambura.

Katika hatua nyingine, Bulaya ametaka hatua zichukuliwe dhidi ya watendaji wa halmashauri ambazo zimebainika kuwa na upotevu wa mabilioni ya fedha za mikopo ya asilimia 10, huku akiwatolea macho wakurugenzi, maafisa maendeleo na mipango.

“Wakati Rais Samia anapokea ripoti ya mikopo ya asilimia 10,alisema fedha ambazo hazijakusanywa zimeongezeka kutoka Sh. 47 hadi 88 bilioni, mchanganuo wake unaambiwa Sh. 900 milioni ni vikundi hewa, Sh. 700 milioni watu wamechukua wakagawana, Sh. 2.5 bilioni vikundi havishughulishi na kazi yoyote,” amesema Bulaya na kuongeza:

“Naomba niwaambie watoaji mikopo ni wakurugenzi, maafisa maendeleo na maafisa mipango, inakuwaje kuna vikundi hewa vinatoa mikopo? Inakuwaje kua vikundi havifanyi biashara? watu wamepewa hela wanagawana, inatakiwa wahusika wachukuliwe hatua.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Biteko: Samia ni muumini wa maridhiano sio kwa kuigiza

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Mpango: Sitakufa bali nitaishi

Spread the loveMAKAMU  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk....

Habari za SiasaTangulizi

Mbowe: Miaka 62 ya uhuru tujenge upya mioyo yetu

Spread the loveWAKATI Tanganyika ikiadhimisha miaka 62 tangu kupata uhuru, Mwenyekiti wa...

Habari za Siasa

Rais Samia asamehe wafungwa 2,244

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewasamehe wafungwa 2,244, huku akiwabadilishia...

error: Content is protected !!