Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Bulaya ataweza kuumeza mfupa uliomshinda Selasini?
Habari za SiasaTangulizi

Bulaya ataweza kuumeza mfupa uliomshinda Selasini?

Spread the love

MBUNGE wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Amos Bulaya, ametangazwa kuwa Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).

Uteuzi huo umefanywa na kiongozi wa kambi hiyo na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Kutangazwa kwa Bulaya kuchukua nafasi ya Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, kunafuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Joseph Selasini.  

Selasini, ambaye ni mbunge wa Rombo (Chadema), alitangaza kujiuzulu wadhifa huo, wiki mbili zilizopita, kufuatia madai ya kutopewa barua ya kutambulishwa kwa uongozi wa Bunge.

Kwa mujibu wa baadhi ya wabunge wa Chadema, kukosekana kwa barua ya utambulisho kwa uongozi wa Bunge, kulimfanya Selasini kufanya kazi yake ya unadhimu katika mazingira magumu sana na kwamba haki zote alizokuwa akipewa ikiwapo haki ya kusimama kama mnadhimu wa upinzani, zilitokana na kuwa na mahusiano mazuri na wabunge wenzake, akiwamo Spika.

Mbowe alimteua Selasini kushika nafasi ya Mnadhimu, siku chache baada ya Mnadhimu wa awali, Tund Lissu, kushambuliwa kwa risasi, akiwa nyumbani kwake, Area D, mjini Dodoma, tarehe 7 Septemba 2017.

Lissu aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, kwa sasa yuko nchini Ubelgiji, akihofia kuja nchini kutokana na kutohakikishiwa usalama wake na tayari ametangazwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kupoteza ubunge wake.

MwanaHALISI limeshindwa kufahamu mara moja, iwapo  Mbowe amepeleka barua ya utambulisho wa Bulaya kwa Spika au Katibu wa Bunge.

Taarifa zinasema, katika kipindi chote cha uongozi wake, Mbowe amewahi kuandika barua moja tu: Ni ile iliyomueleza Spika Ndugai kuwa Magdalena Sakaya (CUF), siyo sehemu ya wabunge wa UKAWA.

“Lakini hata baada ya UKAWA kuvurugika bungeni na wabunge wa CUF kuwekwa kando kinyemela, Mbowe hajawahi kuandika barua kwa Spika Ndugai kumjulisha hilo,” ameeleza mtoa taarifa wa MwanaHALISI.

Akiandika katika ukurasa wake wa twitter, Halima James Mdee, mbunge wa Kawe na ambaye ni “swahiba mkuu” wa Bulaya amesema, kuteuliwa kwa mwanamama huyo, ni ushahidi kuwa wanawake wakipewa nafasi, wanaweza.

Amesema, “hongera sana Ester Bulaya kwa kuteuliwa kuwa Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni. BAWACHA inakupongeza sana. Tunakutakia heri katika wajibu wako mpya.”

Hata hivyo, uteuzi wake unaacha maswali lukuki. Miongoni mwa maswali hayo, ni vigezo vilivyotumika kumteuwa Bulaya kushika nafasi hiyo.

Moja ya kazi kuu ya Mnadhimu wa Bunge, ni kusimamia nidhamu na maadili ya wabunge. Bulaya ni miongoni mwa wabunge wa Chadema, wanaoongoza kwa utovu wa nidhamu, ndani na nje ya Bunge.

Mbunge mmoja wa Chadema ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, ameeleza kuwa kuteuliwa kwa Bulaya kwenye nafasi hiyo, kumethibitisha kuwapo kwa “ombwe la uongozi,” ndani ya chama hicho.

Bulaya aliwahi kusimamishwa ubunge katika mkutano was aba (7), Juni 2017, kufuatia hatua yake ya “kutaka kumpambania,” kinyume cha Kanuni za Bunge, Mdee, ambaye wakati huo, tayari Bunge liliazimia kumsimamisha kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge.

Bulaya na Mdee ambao ni maswahiba wakubwa, walisimamishwa kuhudhuria baadhi ya vikao vya mkutano wa 7 wa Bunge la Bajeti na mkutano wa 8 na wa 9 kwa utovu wa nidhamu (kudharau kiti cha spika).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

error: Content is protected !!