May 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bukoba ‘kuushughulikia’ muswada wa habari

Spread the love

WAANDISHI wa habari mkoani Kagera wameombwa kutoa maoni yao juu ya Muswada wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, anaandika Mwandishi Wetu.

Rai hiyo imetolewa na Bwana Deodatus Balile, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) wakati akiwasilisha muswada wa sheria hiyo kwa waandishi wa habari iliyofanyika leo katika Manispaa ya Bukoba, Kagera.

Balile amesema, ni vyema waandishi wa habari watoe siku maalum ya kuusoma, kuutafakari na kuutolea maoni kabla ya Oktoba 14, mwaka huu.

“Ikumbukwe sheria tunayoiondoa imekaa zaidi ya miaka 40. Sheria hii inayopendekezwa ni nzuri, inalenga kuongeza weledi kwa wanahabari, inaanzisha chombo kitakachoratibu utendaji wa waandishi nchini kitakachojulikana kama Baraza Huru la Habari.

“Sheria inayopendekezwa inao upungufu katika sehemu kadhaa, lakini tunaamini kwa usikivu wa serikali ya sasa hayo machache tutashauriana na yatarekebishika.

“Tunamshukuru waziri mwenye dhamana na masuala ya habari, Mhe. Nape Nnauye amekuwa msikivu katika mchakato huu, na tunaamini waandishi na wadau wa masuala ya habari kote nchini wakitoa maoni yao atatusikiliza na tutafika pazuri kwa kutunga sheria itakayotumika hata miaka 100 ijayo,” amesema Balile.

Amesema, maoni ya wadau yataunganishwa na ya mikoa mingine na kupelekwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii mwezi huu.

Aidha, Balile ameongeza katika kutoa na maoni, ni vyema wadau watoe mapendekezo ya ni jambo lipi wangependa liwemo kwenye sheria hiyo.

Mchakato wa kutunga sheria hii ya Huduma za Vyombo vya Habari, ulianza mwaka 1992 na kwa muda wa miaka 22 ulikwama kutokana na serikali zilizopita kushindwa kuufikisha bungeni.

Machi mwaka jana Serikali ya Awamu ya Nne, ilipeleka muswada huo bungeni chini ya Hati ya Dharura bila kushirikisha wadau, na baada ya kilio cha wadau, serikali haikupata muda wa kuendelea na muswada huo.

Chini ya kanuni za mabunge, Bunge linapomaliza muda wake, miswada yote linayokuwa haijapitishwa inakufa kifo cha asili kwani Bunge la 11 lilipoanza kazi baada ya kuzinduliwa na Rais John Magufuli ilibidi miswada yote iliyoanchwa viporo isomwe upya kwa mara ya kwanza.

Nape, aliyeshirikiana na wataalam wa wizara kurekebisha muswada uliokuwa umewasilishwa chini ya hati ya dharura awali, kurekebisha vifungu vilivyokuwa vinapingana na Sera ya Habari na Utangazaji ya Mwaka 2003.

Katika Bunge lililomalizika Septemba, Nape amewasilisha muswada huu uliorekebishwa ukasomwa kwa mara ya kwanza na sasa umeletwa mikononi mwa wadau kwa ajili ya kuutolea maoni.

Umoja wa Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CORI) kwa kushirikiana na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) ulikutana jijini Dar es Salaam wiki iliiyopita na kuteua Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuratibu kazi hii ya kuchukua maoni ya wadau kuhusiana na muswada huu.

 

 

error: Content is protected !!