September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bugando yaokoa Bil 2 matibabu ya Saratani 

Mtaalam wa mionzi Alex Mpugi akitoa maelezo jinsi mashine ya mionzi inavyofanya kazi

Spread the love

PROFESA Abel Makubi, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC) amesema, hospitali hiyo imefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh. 2 Bilioni kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa kusafiri kwenda Dar es Salaam kupata matibabu ya saratani kila mwaka. Anaripoti Hamis Mguta…(endelea).

Prof. Makubi ametoa kauli hiyo tarehe 7 Agosti 2019, alipozungumza na maofisa habari wa Wizara ya Afya na taasisi zake jijini Mwanza, wakati wa kuonesha mafanikio ya utoaji huduma za afya kwa wananchi.

Amesema, kuanza kwa tiba ya saratani katika Bugando kumesaidia kuokoa kiwango hicho cha fedha kutoka kwa wananchi wa kanda hiyo, na kwamba awali iliwalazimu kwenda Hospitali ya Saratani ya Ocean Road, jijini Dar es Salaam kupata huduma hizo.

“Tunaishukuru Wizara ya Afya  ambayo ilitupatia kiasi cha Shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya kujenga jengo  la saratani. Kama hospitali  tumeweza kununua  mashine nne za mionzi na dawa kwa kushirikiana na wafadhili wengine,”amesema.

Amesema, hivi sasa asilimia 90 ya wagonjwa hawapelekwi Dar es Salaam hivyo wanapata huduma ndani ya kanda, awali zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa wa saratani wa Ocean Road walikuwa wakitoka kanda hiyo.

Alex Mpigi, ambaye ni Mtaalam wa Tiba Mionzi wa Idara ya Saratani wa BMC amesema, kabla ya mashine hizo walikua wakitoa huduma za saratani kwa kutumia kemikali.

“Naomba nitoe wito kwa wananchi hususan wanawake kujitokeza kufanya uchunguzi wa saratani ya shingo ya uzazi na matiti kila siku ya Jumanne na Alhamis,” amesema.

Dk. Fabian Massaga, Mkurugenzi wa Upasuaji amesema, hospitali hiyo imefanikiwa kufanya ukarabati na upanuzi wa vyumba vya upasuaji, kutoka vyumba sita hadi 13 ambapo vyumba viwili hutumika kwa upasuaji wa dharura na kimoja kwa ajili ya upasuaji  kwa akina mama wajawazito.

“Upande wa upasuaji  tumeweza kuongeza idadi ya wagonjwa kutoka 25 hadi 50 na hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wengi waliokuwa wanasubiri upasuaji kwa miezi mitatu, lakini hivi sasa wanafanyiwa upasuaji ndani ya wiki moja,”amesema.

Dk. Massaga amesema, upanuzi huo umeendana na ununuzi wa vifaa vipya na vya kisasa  ikiwemo vitanda vya kufanyia upasuaji, taa maalumu za vyumba vya upasuaji na mashine za kisasa kabisa za kutolea dawa ya usingizi.

Vifaa hivi vimeagizwa moja kwa moja viwandani kwa takribani Shilingi bilioni 1.4 badala ya Shilingi bilioni 3 kama wangenunua kwa wauzaji hapa nchini.

error: Content is protected !!