BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeongeza muda wa siku 30 wa usimamizi wa Yetu Microfinance Bank Plc baada ya mchakato wa kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa matatizo ya taasisi hiyo ya kifedha kutokamilika. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hatua hiyo inakuja baada ya tarehe 12 Disemba 2022 BoT kusitisha shughuli za utoaji wa huduma za kibenki za Yetu Microfinance Bank Plc kwa muda wa siku 90 ili kuipa nafasi Benki Kuu ya Tanzania kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa suala hili.
Hata hivyo katika taarifa iliyotolewa leo tarehe 14 Machi 2023 na Gavana wa BoT, Emanuel Tutuba imesema muda wa usimamizi umeongezwa kwa kipindi cha siku 30 kuanzia tarehe 12 Machi 2023.
“Itakumbukwa kwamba, kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha sheria namba 56(1)(g)(iii) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ya Tanzania iliamua kuchukua usimamizi wa Yetu Microfinance Bank Plc kuanzia tarehe 12 Disemba 2022 baada ya kubaini kuwa ilikuwa na upungufu mkubwa wa ukwasi na mtaji kinyume na matakwa ya sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake.
“Baada ya kuchukua usimamizi wa benki hii, Benki Kuu ya Tanzania ilisitisha shughuli za utoaji wa huduma za kibenki za Yetu Microfinance Bank Plc kwa muda wa siku 90 ili kuipa nafasi Benki Kuu ya Tanzania kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa suala hili,” imesema taarifa hiyo.
Aidha, BoT imeuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.
Leave a comment