BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa onyo kwa wananchi wanaodhihaki na kukejeli fedha ya nchi, kwa kuwa kitendo hicho ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa jana tarehe 18 Septemba 2018 na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki baada ya hivi karibuni kutokea matukio ya ya baadhi ya wananchi kuzifanyia dhihaka na kebehi noti za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzirusha hovyo na kucheza huku wakizikanyaga.
Siku kadhaa zilizopia, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilimkamata mwanamuziki wa Bongo Fleva nchini Maua Sama pamoja na mtangazaji Soud Brown kwa kosa la uharibifu wa mali, baada ya kuonekana video katika mitandao ya kijamii ikimuonyesha mwanamuzi huyo akicheza huku akikanyaga fedha.
“BoT imewataka wananchi kuheshimu fedha ya Tanzania kwa kuwa ni moja ya alama ya taifa na kuonya kwamba kudhihaki na kukejeli noti na sarafu za Tanzania ni kosa la jinai.
“Onyo hilo limetolewa leo (jana) kufuatia matukio ya hivi karibuni ya baadhi ya wananchi kutoziheshimu na kuzifanyia dhihaka na kebehi noti za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzirusha hovyo na kucheza huku wakizikanyaga kana kwamba ni karatasi za kawaida zisizoheshimika,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, jambo hilo ni dharau kwa serikali inayotumia gharama kubwa katika utengenezaji wa noti hizo. Na kwamba ni kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu namba 332A cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Penal Code) Sura ya 16 kamailivyorejewa mwaka 2002.
“Benki Kuu inapenda kuchukua fursa hii kuwatahadharisha wananchi kutojihusisha na vitendo vya aina hii, endapo ikibainika hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayehusika.
“Benki Kuu inatoa rai kwa wananchi kuzitunza fedha zetu kwa kuwa ni mojawapo ya tunu na alama muhimu ya uchumi wa nchi yetu. Vilevile, utunzaji mzuri wa fedha zetu utapunguza uwezekano wa fedha hizo kuchakaa mapema na gharama za uchapishaji,” ilisisitiza taarifa hiyo.
Leave a comment