Spread the love

 

MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amemuagiza meneja wa TARURA Mkoa wa Katavi, Mhandisi Innocent Mlay kujenga daraja la muda kwa haraka ili wananchi wasipate usumbufu kupita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Katavi … (endelea).

Ni baada ya Daraja la Kaseke linalounganisha Vijiji vya Kaseke, Mbugani na Itenka Kata ya Kaseke, Mpanda mkoani humo kuharibiwa na mvua.

Mhandisi Seff ametoa maagizo hayo leo Alhamisi, tarehe 19 Mei 2022, katika ziara yake mkoani Katavi na kukuta wananchi wakilipishwa kiasi cha kati ya Sh.100- 500 kwa siku kuvuka katika kivuko kilichojengwa na baadhi ya wanakijiji.

Amewataka kusitisha mara moja tozo wanayowalipisha wananchi na kumuagiza Mhandisi Mlay kurudisha gharama ya Sh.1,500,000 waliyodai ni fedha iliyotumika kujenga kivuko hicho ili wananchi wavuke bila kulipa.

“Nimesikitishwa kuona wananchi hasa wakinamama wanalipishwa kuvuka hapa, sasa msitishe mara moja kuwalipisha na meneja atarudisha hizo gharama mlizosema,” alisema Mhandisi Seff.

Aidha amemuagiza meneja Mkoa kujenga daraja la muda kwa haraka wakati ufumbuzi wa kujenga daraja la kudumu unafanyiwa kazi.

“Kama mnavyoona uharibufu uliotokea hapa ni mkubwa hivyo daraja la kudumu litachukua muda kidogo, tutajenga daraja la muda ili muweze kuvuka kwa usalama zaidi, “ amesema Mhandisi Seff.

Kwa upande wao, wananchi wa Kaseke wameushukuru uongozi wa TARURA kwa kutembelea eneo hilo na kuleta suluhisho la adha kubwa walizokuwa wanazipata.

“Tunakushukuru sana kiongozi ulivyofika hapa, kwa kweli adha tunazopata ni kubwa sana, wakinamama hapa tunapata shida ya kwenda zahanati na watoto na tukivuka hapa tunalipishwa, sasa tunafurahi umesema tusilipe na pia mnatujengea daraja hilo la muda,“ alisema Elizabeth Milambo, mkazi wa Kaseke.

Naye Neema Msemakweli alisema anaishukuru Serikali kwa kuwatembelea na kuahidi kuwajengea daraja la muda litakalowwndole kero walizokuwa wakipata hasa mvua inaoinyesha.

“Hapa tulikuwa tukipata taabu sana kuvuka kwenda mashambani mvua zikinyesha na bado tulikuwa tukilipa shilingi 500 hadi 1000 tumefarijika mmekuja na tunamwomba mama Samia Rais wetu ambaye tunajua anatujali wanawake daraja la kudumu kumaliza kabisa tatizo la hapa,“ alisema Neema.

Kwa upande wake, Innocent Janson, mkazi wa kijiji cha Mbugani, alisema anaomba viongozi waendelee kuwajali wananchi wanyonge kwa kutatua kero zao kwa kuwatembelea katika maeneo yao ili kuona hali halisi ya matatizo yao na alishukuru sana kwa ujio wa mtendaji mkuu wa TARURA na kutoa Suluhu ya kero zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *