May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bosi SADC kustaafu, Rais Samia amkaribisha nyumbani

Spread the love

 

DAKTARI Stergomena Tax, Agosti 2021, atamaliza muda wake wa utumishi wa miaka nane wa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) huku Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akimkaribisha nyumbani. Anaripoti Jemima Samwel, DMC…(endelea).

Dk. Tax ambaye ni raia wa Tanzania, alianza kutumikia jumuiya hiyo mwaka Septemba 2013, baada ya kuteuliwa katika mkutano wa 33 wa SADC uliofanyika, Lilongwe nchini Malawi.

Hayo ameyasema leo Ijumaa, tarehe 23 Aprili 2021, alipofanya mazungumzo na Rais Samia, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma. Dk Tax amempa taarifa juu ya masuala mbalimbali yahusuyo SADC.

Katika maungumzo hayo yaliyohudhuliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Balozi Liberata Mulamula, Dk. Tx amempongeza Rais Samia kwa kushika madaraka ya urais na kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania.

Pia, amempongeza kwa hotuba nzuri aliyoitoa jana Alhamisi Bungeni jijini Dodoma, iliyotoa mwelekeo wa serikali ya awamu ya sita, uliyoingia madarakani tarehe 19 Machi 2021.

Samia aliapishwa kuwa rais baada ya kifo cha Rais John Pombe Magufuli, tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam na mwili wake, kuzikwa nyumbani kwao, Chato mkoani Geita.

Dk. Tax ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano alioupata wakati wote akiwa katibu mtendaji wa SADC na ameipongeza Tanzania ambayo wakati wa uenyekiti wake wa SADC, imeandaa na kukamilisha mkakati wa maendeleo wa SADC licha kuwepo kwa changamoto za janga la corono duniani.

Amesema, imefanikiwa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya SADC, kuanza mradi wa uwekaji sanamu ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika Umoja wa Afrika (AU) na uendelezaji wa gesi.

Aidha, amesema katika kipindi hicho SADC imeendelea kuwa na utulivu wa kisiasa ambao umetoa fursa nyingi za maendeleo ya kiuchumi, hivyo ametoa wito kwa Tanzania kutilia mkazo katika uimarishaji wa sekta za uzalishaji kama vile viwanda, kilimo, biashara, kusimamia ubora na kuendeleza miundombinu.

Kwa upande wake, Rais Samia amempongeza Dk. Tax kwa kuiwakilisha vizuri Tanzania katika utumishi wake akiwa katibu mtendaji wa SADC na ameahidi kufanyia kazi ushauri na fursa mbalimbali ambazo SADC anazitoa kwa Tanzania.

Rais Samia amemkaribisha nyumbani, Dk. Tax, baada ya kumaliza muda wake ili aungane na Watanzania katika ujenzi wa Taifa.

Dk. Tax, amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afrika Mashariki ya Tanzania kati ya Novemba 2008 hadi August 2013, ikiwa ni katika utawala wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

error: Content is protected !!