June 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bosi NIDA ashikwa maradhi Rumande

Spread the love

DICKSON Maimu, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ameshindwa kufika mahakamani kutokana na maradhi, anaandika Faki Sosi.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, Maimu anakabiliwa na mashtaka 27 ya uhujumu uchumi na kusababisha hasara ya Sh.1.16 Bil.

Taarifa za kuumwa kwake zimezotolewa na Leornad Swai, Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mbele ya Rescpicius Mwijage, Hakimu Mkazi Mkuu.

Wakili Swai amedai kuwa, shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa lakini mshtakiwa wa kwanza (Maimu) ameshindwa kutokea mahakamani kwa sababu anaumwa, pia upelelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo anaomba apangiwe tarehe nyingine.

Baada ya kueleza hayo, hakimu Mwijage aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe 14 Septemba, mwaka huu.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Avelin Momburi, Meneja Biashara wa NIDA; Joseph Makani, Mkurugenzi wa TEHEMA; Benjamin Mwakatumbula, Kaimu Mhasibu Mkuu wa NIDA; Astery Ndege, Mkurugenzi wa Kampuni ya Bima ya Aste Insurance Brokers; George Ntalima, Ofisa Usafirishaji; Sabina Raymond, Mkurugenzi wa Sheria na Xavery Kayombo.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia madaraka vibaya, kula njama, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. 1.169 Bilioni.

Shitaka la kwanza linamkabili Maimu na Mwakatumbula ambao wanadaiwa kwa tarehe tofauti kati ya tarehe 15 hadi 19 Januari, mwaka 2010 katika Makao Makuu ya NIDA wilayani Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nafasi walizokuwa nazo walitumia madaraka vibaya.

Walidaiwa kuwa, waliidhinisha malipo kwa Gotham International Limited (GIL) ya Dola za Marekani 2,700,00 bila kutumia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni vilivyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania kinyume na kifungu 19.3 cha mkataba kati ya NIDA na GIL hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh. 3,969,000.

Mshtakiwa Maimu na Mwakatumbula katika shitaka jingine wanadaiwa kati ya Juni 3 na 5, 2013 katika Makao Makuu hayo walitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani milioni 1.8, bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 106,346,000.

Washtakiwa hao wawili wanadaiwa Juni 20, 2014 katika Makao Makuu hayo, waliidhinisha tena malipo ya Dola za Marekani 675,000 kwa GIL bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 42,471,000.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo mengine ya Sh 6 Milioni kwa GIL bila ya kupiga hesabu kwa kutumia viwango vya kubadilishia fedha hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh. 14, 661,676.76.

Mbagwa alidai Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari 15, 2010 na Mei 16, 2015 katika Makao Makuu hayo ya NIDA kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni waliisababishia NIDA kupata hasara ya Sh. 167,445,676.76.

error: Content is protected !!