Tuesday , 26 September 2023
Home Habari Mchanganyiko Bosi NIC apandishwa kizimbani, akabiliwa na mashitaka 365
Habari MchanganyikoTangulizi

Bosi NIC apandishwa kizimbani, akabiliwa na mashitaka 365

Spread the love

 

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Samwel Peter Kamanga na wenzake sita, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa na kusomewa mashitaka 365 yakiwamo ya utakatishaji wa fedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mashitaka mengine, ni kuongoza genge la kiharifu, kujipatia fedha kiasi cha Sh. 1.8 bilioni, mali ya shirika hilo, kinyume cha sharia; kuchepusha fedha, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Aidha, vigogo hao wa NIC wanashitakiwa kwa makosa ya kughushi, kutoa nyaraka za uongo na kulisababishia shirika hilo la umma hasara ya mabilioni ya shilingi.

Hata hivyo, waendesha mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Ipyana Mwakatobe na Grace Mwanga, waliishia kuwasomea washitakiwa hao mashitaka 101, kabla ya Mahakama kuahirisha shauri hilo hadi tarehe 5 Juni (Jumatatu ijayo).

Kesi dhidi ya watuhumiwa hao, imesomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi.

Kamanga aliyeteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa NIC, tarehe 26 Oktoba 2016 na aliyekuwa rais wa Jamhuri, Dk. John Pombe Magufuli, uteuzi wake ulifutwa, 29 Julai 2019.

Washitakiwa wote saba, wamepelekwa gerezani, kutokana na baadhi ya mashitaka, likiwamo la utakatishaji fedha, kutokuwa na dhamana kwa sheria za Tanzania.

Kabla ya uteuzi huo, Kamanga alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NIC. Nafasi yake, ilikabidhiwa kwa Elirehema Doriye, ambaye ndiye anashikilia wadhifa huo hadi sasa.

Washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo, ni aliyekuwa kaimu mhasibu mkuu wa shirika, Tabu Kingu; pamoja na wahasibu Victor Mleleu, Peter Nzunda, Kenan Mpalanguro, Lisubilo Sambo na Mfworo Ngereja.

Katika shitaka la kuongoza genge la uhalifu, mahakama imeelezwa kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo kati ya tarehe 1 Januari 2013 na 31 Desemba 2018, katika maeneo tofauti tofauti jijini Dar es Salaam, Rukwa, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Morogoro na Kigoma.

Inadaiwa katika kipindi hicho, washitakiwa kwa pamoja na kwa makusudi, waliongoza genge la uhalifu na kujipatia kiasi cha Sh. 1,863,017,400.76, kwa njia ya udanganyifu, kutoka shirika hilo ambalo ni mali ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

NIC lilikuwa moja ya shirika kubwa la bima nchini, katika miaka ya sitini hadi tisini. Lilianza kuteteleka mwanzoni mwa mwaka 2000, kutokana na uongozi mbovu wa wakurugenzi walioongoza shirika hilo, ukimuondoa Gibbons Mwaikambo.

Waliongoza NIC baada ya Mwaikambo na ambao wanatajwa kuwa ni kiini cha kuteteleka kwa shirika, kutokana na uongozi wao mbovu, ni pamoja na John Chimile Lubambe, Bakari Mwapachu, Octavian Temu, Margert Ikongo, Justine Mwandu na Kamanga mwenyewe.

Mwandu kwa sasa, ndiye mwenyekiti wa Bodi ya NIC. Uteuzi wake, uliibua malalamiko na manung’uniko lukuki, kutoka kwa baadhi ya wadau wa masuala ya bima, wakiwamo waliokuwa wafanyakazi wa shirika hilo.

Aidha, NIC – shirika lililokuwa na udhibiti wa asilimia 99 wa soko la bima nchini mwaka 1997 –   lilipomoroka hadi kushikilia udhibiti wa chini ya asilimia 30 katika miaka ya hivi karibuni.

Wachambuzi wa mambo wanasema, mporomoko huu wa haraka, haukuletwa na ushindani wa makampuni mengine ya bima yaliyoanzishwa, bali umetokana na baadhi ya viongozi wake, kujihusisha na vitendo vya rushwa, ghiliba na udanganyifu.

Maelfu ya mali za shirika zilizotapakaa nchi mzima, ziliuzwa kwa bei ya kutupwa na mithili ya mali iliyokuwa na mwenyewe, huku baadhi ya waliokuwa watendaji wake wakuu, wakiwa ndio wanufaikaji wakubwa.

Miongoni mwa mali za NIC zilizouzwa, ni pamoja nyumba za wafanyakazi zilizokuwapo Tabata, Mikocheni na Kijitonyama, jijini Dar es Salaam; jijini Mbeya, Arusha, Bukoba na Mwanza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Chande aliyeng’olewa TANESCO kwenda TTCL apelekwa Posta

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua aliyekuwa, Mkurugenzi Mkuu wa...

Habari Mchanganyiko

Rais Samia apewa tano ujenzi barabara Mtwara

Spread the loveWANANCHI wa Mkoa wa Mtwara, wameishukuru Serikali ya Rais Dk....

BiasharaHabari Mchanganyiko

Serikali kununua mitambo 15 ya kuchoronga miamba

Spread the loveSerikali kupitia Wizara ya Madini imepanga kununua mitambo 15 ya...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Mtanzania aweka rekodi kimataifa kwa kiwanda cha kusafisha dhahabu

Spread the loveIMEELEZWA kuwa Kiwanda cha Kusafisha dhahabu cha Geita Gold Refinery...

error: Content is protected !!