December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bosi kituo cha Polisi Tazara awakana kina Mbowe

Spread the love

 

INSPEKTA Rugawa Issa Maulid (42), Kaimu Mkuu wa Kituo cha Polisi Tazara, amekata kufikishwa kituoni hapo kwa watuhumiwa wa kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Maulid, ambaye ni shahidi wa nne wa Jamhuri, amedai hayo wakati akitoa ushahidi leo Jumatano, tarehe 24 Novemba 2021, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, iliyopo Mawasiliono jijini Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Ni katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa, Mohammed Abdillah Ling’wenya yasipokelewe mahakamani kama kilelezo wakidai hayakutolewa na mshtakiwa huyo bali alilazimishwa kusaini karatasi iliyodaiwa kuwa na maelezo yake.

Shahidi huyo ametoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando akidai Ling’wenya na mwenzake Adam Kasekwa, hawakufikishwa kituoni hapo, kama inavyodaiwa na watuhumiwa hao.

Washtakiwa hao walitoa madai hayo katika kesi ndogo ya kwanza ya kupinga maelezo ya onyo ya Kasekwa, ambapo walidai baada ya kukamatwa tarehe 5 Agosti 2020 na kuwekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro, walisafirishwa na kuwekwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Tazara.

Inspekta Rugawa amekanusha madai hayo, baada ya Ling’wenya na mwenzake kudai mahakamani hapo, walifikishwa Tazara.

Mahojiano yao yalikuwa kama ifuatavyo;

Kidando: Unafanyia kazi ofisi ipi?

Shahidi: Kituo cha Polisi Tazara

Kidando: Una nafasi gani pale kituoni?

Shahidi: Kwa sasa ni kaimu Mkuu wa Kituo

Kidando: Eneo lako la kazi ni lipi?

Shahidi: Eneo langu la kazi ni kuanzia Dar es Salaam mpaka Kisaki, wilaya ya Morgoro Mjini eneo ninalokaimu mimi kama mkuu wa kituo.

Kidando: Elezea mahakakani nafasi hiyo ya kaimu mkuu wa kituo umeipata lini?

Shahidi: Nakumbuka nilikabidhiwa majukumu hayo tarehe 3 Juni 2021

Kidando: Majukumu yako nini?

Shahidi: Majukumu yangu yamegawanyika sehemu kuu tano, kwanza kusimamia ndihamu za askari ninaowaongoza, kusimamia na kulinda mali zote za serikali yakiwemo majengo kituo chenyewe, kusimamia mpango kazi wa kituo, kusimamia doria, kuhakikisha askari wameingia kazini kwa wakati na maeneo husika waliyopangiwa.

La tano, kusimamia mahabusu wote walioko kituoni, kuhakikisha wako salama koafya kwa kuoata huduma za chakula ipasavyo.

Kidando: Baada ya kuchukua Detention Register (DR) unafanya nini?

Shahidi: Lazima niongozane na askari mmoja au wawili kuelekea mahabusu kama kuna watuhumiwa wa kike nakuwa na askari mmoja wa kike na mmoja wa kiume nafika mahabusu nafungua mahabusu nachukua DR nafungua kwa tarehe husika naanza kuita majina ya mmojammoja ambao wameandikwa kwenye kitabu hicho.

Kidando: Dhumuni ni nini?

Shahidi: Dhumuni kutambua kitu kilichoandikwa kwenye dentention register kinafanana na reality na phisical check up

Kidando: Baada ya kukagua na kujiridhisha unafanya nini?

Shahidi: Najiridhisha walioko kwenye selo na detention register ni hawa, nafunga selo na kurudi charging office, baada ya kufika nasaini kwamba nimeikagua nawakabidhi watu wa charging office kuendelea na majukumu yao.

Kidando: Malengo ya kufanya ukaguzi mahabusu ni nini?

Shahidi: Malengo kwanza kuoanisha taarifa zilizopo kwenye kitabu na mahabusu walioko selo pili kufuatilia mwenendo wa upelelzi je hao mahabusu wapelelzi nimewa-sign kupeleleza kesi zao wametekelza majukumu yangu ikiwa kukamilisha upelelezi. Kama wamekamilisha upelelezi nawaamuru mtuhumiwa afikishwe mahakamani kwa wakati na kama upelelezi haujakamilika nawaamuru upelelezi ukamilike.

Kidando: Elezea mnamo mwezi Agosti 2020, katika majukumu yako ya askari ulikuwa wapi?

Shahidi: Nakumbuka kabla tarehe 3 Agosti 2020 kuanzia Mei 2020 nilikuwa Operesheni Ofisa wa Kikosi cha Polisi Tazara, kuanzia tarehe 10 Mei 2020, nilikuwa nahudumu kuanzia Dar es Salaam mpaka Tunduma boda.

Kidando: Na ulikuwa unatekeleza majukumu gani?

Shahidi: Majukumu niliyokuwa nayo kama operesheni ofisa kwanza kuhakilisha treni zote zinazotembea lazima kuwepo askari waliopangwa kwa wakati huo na kwa idadi wanaotakiwa. Askari kwa ajili ya kusimamia usalama wa mali pamoja na abiria.

Kupata taarifa za mahabusu waliokuwepo kituoni baada ya kupata taarifa za mahabusu tulio nao nazifikisha kwa kamanda wa polisi

Kidando: Ulikuwa unatekeleza majukumu gani Agosti 2020?

Shahidi: Nakumbuka tarehe 2 Agosti 2020, nilipewa barua na kamanda wa kikosi nikakaimu majukumu ya kukaimu mkuu wa Kituo cha Tazara Pugu Road, baada ya aliyekuwepo kwenda likizo fupi ya siku 28.

Kidando: Baada ya kupata barua, majukumu hayo uliyaanza lini na yaliishia lini?

Shahidi: Nilianza rasmi 3 Agosti 2020 mpaka tarehe 6 Septemba 2020

Kidando: Huyu aliyeenda likizo alikwua nani?

Shahidi: Inspekta Richard Ogutu

Kidando: Katika shughuli kusimamia ni kitu gani kama kaimu ulikifanya?

Shahidi: Kuna kitabu cha kufungua taarifa za kesi zote zinafunguliwa kituoni, pili kuna detention register niliyozungumzia mwanzo, tuna kitabu kinachoonesha mali anazomiliki mtuhumiwa baada ya kufanya upekuzi.

Kidando: Katika kipindi ambacho ulikuwa unakamu elezea mahakamani tarehe 7,8,9, Agosti 2020, ulikuwa wapi na unatekelza majukumu ganu?

Shahidi: Nilikuwa kazini kama kawaida nikitekelza majukumu yangu kama kaimu mkuu wa kituo cha Polisi Tazara

Kidando: Elezea mahakamani katika kipindi cha hizo siku tatu kama ulifanya shughuli yoyote?

Shahidi: Nakumbuka tarehe 7 nilifanya ukaguzi wa mahabusu, katika mahabusu hakukuwa na mtuhumiwa hata mmoja, tarege 8 nilifanya ukaguzi kama kawaida, palikuwa na mtuhumiwa mmoja.

Tarehe 9 palikuwa na watuhumiwa wawili wanafunzi walikuwa wanatuhumiwa kuhatarisha miundombinu ya reli, tuliwakamata wakifungua reli.

Kidando: Ulibaini vipi uwepo wa hawa watuhumiwa tarehe 8 na 9 Agosti 2020?

Shahidi: Kama zilivyotaratibu inapofika asubuhi lazima nipitie detention register, naziangalia baada ya kuzingalia namchukua mtu wa CRO kuangalia mahabusu na kufanya phisical check up.

Kidando: baada ya kufanya shughuli za kuangalia mahabusu na kubaini uwepo w a2tauhumwia hao wewe una uthibitisho gani kama kweli walikwuepo?

Shahidi: Uthibitisho wangu ni wa detention register watu hao wali-apear kwenye detention register.

Kidando: Hiyo detention register unayosema ina uthibitisho huo, kwa kipindi hiko ilikuwa inatuznwa wapi?

Shahidi: Kipindi hiko mara nyingi inakuwa charging office, kwa hiyo ilikuwa charging office

Kidando: Hiyo tarehe 6 Septemba 2020 nini ilitokea ambapo unasema uliendelea kukaimu?

Shahidi: Alikuja Richard Ogutu, nilimkabidhi mali zote ambazo ziko kwenye kituo , silaha za moto, magari pamoja na kituo kikiwa salama na mahabusu na nyaraka nyingine za siri za Serikali.

Kidando: Unakaimu nafasi kutoka kwa nani?

Shahidi: Richard Ogutu ambaye amehamishiwa Zanzibar

Kidando: Baada kuhamishiwa Zanzibar, elezea kitu gani kilitokea tarehe 3 Juni 2021, lini ulikabidhiwa majukumu haya?

Shahidi: tarege 3 Juni 2021

Kidando: Nani aliyekukabidhi majukumu hayo?

Shahidi: Richard Ogutu

Kidando: Makabidhiano hayo yalifanyikaje?

Shahidi: Kupitia nyaraka

Kidando: Detention Register uliyoitumia Agosti 2020 uliipelekwa wapi?

Shahidi: Nilikuta ilikuwa imekabidhiwa kwenye ofisi yake.

Kidando: Baada ya tarehe 3 lini ulikuja kuifanyia kazi detention register?

Shahidi: Nakumbuka tarehe 14 Novemba 2021 alikuja mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni askari polisi alijitambulisha kwa jina la Inspekta Swilla kutoka ofisi ya DCI

Kidando: Alikuka wapi?

Shahidi: Kituo cha Polisi Tazara alikuja charging toom office Tazara, saa 5 asubuhi, akamuulizia mkuu wa kituo, mimi nikiwa ofisini kwangu alikuja askari toka CRO akasema Inspekta Swilla anakuhitaji

Kidando: Baada ya kupata taraifa hiyo askari anakuhitaji ulichukua hatua gani?

Shahidi: Nilitoka ofisini kwangu na kwenda charging office na kuonana naye ana kwa ana.

Kidando: Baada ya kuonana naye nini kiliendelea?

Shahidi: Alinihoji kuhusu detention register iliyotumika tarehe 7,8,9 Agosti 2020.

Kidando: Alikueleza nini?

Shahidi: Alinieleza nahitajika mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi

Kidando: Ulifanya nini baada ya kukueleza?

Shahidi: Akasema ile detention register ya Agosti ilikuwa imekwisha tangu mwezi mei 2021 nakumbuka tarehe 26 mwisho kutumika kwa hiyo, kwa wakati huo haikuwapo charging room office.

Kidando: Ulifanya nini?

Shahidi: Baada ya kuangalia pale haipo nilimjulisha nitakwenda kuitazama kwenye ofisi yangu ya kumbukumbu, yeye akaondoka na mimi nikarudi ofisini.

Tarehe alizonitajia nilifanya check up, baada ya kuikagua nilikuta tarehe 8 alikuwa mtuhumiwa mmoja, tisa wawili na saini yangu niliyoiweka.

Kidando: Vipi kuhusu tarehe saba?

Shahidi: Katika ukaguzi wangu wa detention register kuanzia tarehe 5, 6, 7 hakukuwa na mahabusu aliyerekodiwa kwenye detention register

Kidando: Hapa mahakamani kuna kesi na nitakutajia majina ili uelezee kama katika hizo tarehe 7, 8, 9 Agosti na useme kama majina yalikuwepo kuna jina la Halfan Hassan Bwire, Adam Hassan Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya?

Shahidi: Kupitia detention register ya tarehe hizo, majina hayo hayakuwepo na watuhumiwa hao hawakuwepo mahabusu.

Kidando: Baada ya hapo uliipeleka wapi?

Shahidi: Baada ya hapo niliihifadhi mpaka nilipokuja hapa nimekuja nayo.

Inspekta Rugawa ni shahidi wa nne kati ya sita waliopangwa kuitwa na jamhuri katika kesi hiyo ndogo, akitanguliwa na Askari Mpelelezi H4347 Goodluck, Askari Mpelelezi Ricardo Msemwa na Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru, mkoani Kilimanjaro, SP Jumanne Malangahe.

Mashahidi hao wa upande wa mashtaka waliieleza mahakama hiyo namna Ling’wenya na mwenzake Adam Kasekwa, walivyokamatwa maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro, tarehe 5 Agosti 2020, kwa kosa la kula njama za kupanga vitendo vya kigaidi.

Pia, waliieleza mahakama hiyo namna na sababu za watuhumiwa hao kutolewa mkoani Kilimanjaro kuja kuhojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, kisha kuhamishiwa Kituo cha Polisi Mbweni, mkoani humo.

Walidai, mhumiwa huyo hakuteswa na wala hakulazimishwa kusaini karatasi yenye maelezo ya onyo kama inavyodaiwa na mawakili wa utetezi, bali alitoa maelezo hayo kwa hiari yake.

Shahidi huyo anaendelea kutoa ushahidi wake mahakamani hapo. Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa taarifa na habari mbalimbali.

error: Content is protected !!