November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bondia afariki kwa kushushiwa makonde ulingoni

Bondia, Taurai Zimunya kabla ya pambano lake

Spread the love

 

MASWALI yameibuka kuhusu usalama wa mchezo wa masumbwi nchini Zimbabwe baada ya Bondia mmoja chipukizi mwenye umri wa miaka 24 kupoteza maisha kutokana na makonde aliyoshushiwa na mpinzani wake kwenye pambano moja jijini Harare. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Bondia huyo Taurai Zimunya amefariki duniani mapema wiki hii tarehe 1 Novemba mwaka huu muda mfupi baada ya kudundwa na Bondia Tinashe Majoni anayetoka katika akademi ya Charles Manyuchi.

Pambano hilo la uzito wa Super bantam lililokuwa la raundi tisa, lilipigwa Jumapili jioni tarehe 31 Oktoba, 2021, lakini ilipofika raundi ya tatu, Zimunya alianguka na kupoteza fahamu.

Hata hivyo, alipokimbizwa katika hospitali ya Parirenyatwa alibakia kwenye hali ya koma na siku iliyofuata akatangazwa kuwa amepoteza maisha baada ya damu kuvujia kwenye ubongo.

Tukio hilo limeibua maswali baada ya video ya bondia huyo iliyosambaa mitandaoni kuonesha akidundwa huku akiwa hajiwezi lakini refa wa mchezo huo hakusimamisha pambano hadi Zimunya alipoanguka chini.

Akizungumzia tukio hilo, Katibu mkuu wa Bodi ya Kitaifa ya Udhibiti wa ndondi na mieleka  nchini Zimbabwe (ZNBWCB), Lawrence Zimbudzana amesema taratibu za uchunguzi kuhusu tukio hilo zinaendelea.

Bondia, Taurai Zimunya kabla ya pambano lake

“Kwa sasa tunashughuliki kukamilisha taratibu za mazishi, kisha tuketi na kuangalia masuala ya mchezo wenyewe,” Zimbudzana aliambia BBC Sport Africa.

Taarifa iliyotolewa na ZNBWCB ilisema “Taratibu zote muhimu za matibabu zilifuatwa na msaada wa dharura wa matibabu ulitolewa ulingoni hapo kabla ya bondia huyo kupelekwa hospitali”.

Zimunya alipigwa makonde kadhaa kichwani kabla ya kutolewa nje ya ulingo katika pambano hilo lisilokuwa na ubingwa.

Aliyekuwa mkufunzi wake Tatenda Gada ameeleza kusikitishwa na kifo cha bondia wake na kuongeza kuwa Zimbabwe imempoteza nyota wa mchezo huo kwani alikuwa na uwezo mkubwa.

“Tumepokonywa mojawapo ya matarajio yetu mazuri, nilifanya kazi na Taurai kwa zaidi ya miaka minne… nilimtazama akistawi katika mchezo huu, alikuwa mmoja wa nyota wajao katika fani hii,” amesema.

Baba yake Zimunya, Samson amesema mwanawe alikuwa bondia mahiri, alitarajia mtoto wake angebeba jina la ukoo kwa kuwa bingwa.

Hii ni mara ya kwanza kwa bondia kufariki nchini Zimbabwe kutokana na majeraha aliyoyapata ulingoni.

Mchezo wa ndondi ulikuwa umerejea nchini Zimbabwe baada ya masharti ya kupambana na janga la Corona kulegezwa.

error: Content is protected !!