WIZARA ya Maji na Umwagiliaji kupitia Bonde la Wami Ruvu inakusudia kutangaza eneo hilo kama hifadhi ya vyanzo vikuu vya maji nchini, anaandika Christina Haule.
Endapo eneo hilo litatangazwa kama hifadhi kutasaidia kulinda na kutunza mazingizra ili liendelee kutoa maji ya uhakika.
Ofisa kutoka Bonde hilo, Grace Chitanda amesema hayo leo hii wakati akiongea na waandishi wa habari na kwamba uhifadhi huo tayari wameshaanza katika eneo la Makotopola mkoani Dodoma na wanatarajia kuendelea katika maeneo mengine.
Amesema uhifadhi huo wa vyanzo vya maji utasaidia kurejesha hali ya uoto wa asili katika vyanzo hivyo na hivyo kuwa kivutio.
Aidha amesema kwa mkoa wa Morogoro wanatarajia kutangaza kuwa hifadhi katika Bwawa na la Mindu na maeneo mengine oevu yenye vyanzo vikuu vya maji.
Ameongeza kuwa shughuli za kibinadamu zinazofanywa kwenye vyanzo vya maji mara nyingi zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa kuharibu na hatimaye hata kukausha vyanzo vya maji na hivyo uhifhadhi huo utasaidia kuleta maana.
Hata hivyo amesema kabla ya kuchukua uamuzi wa kufanya hifadhi wanatekeleza sheria zilizopo za uhifadhi wa maji ili kuweza kuwakamata watakaohusika na uharibifu wa vyanzo vya maji.
“Kwa mfano mtu akifanya shughuli zozote za kibinadamu jirani na vyanzo vya mji ndani ya mita 60 kuanzia chanzo cha maji atafungwa ama atalipa faini isiyopungua Sh. milioni 10,” amesema Chitanda.
Naye Mkuu wa Maabara ya maji mkoani Morogoro, Peter Mhina, amesema uhifadhi huo unapaswa kufuatwa ili kulinda watumiaji na viumbe hai visiweze kupata madhara yoyote.
Leave a comment