January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bomoabomoa ‘yaanza’ Mwanza

Spread the love

WAKATI zoezi la bomoabomoa likiendelea Dar es Salaam, zoezi hilo linatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia sasa jijini Mwanza baada ya watalaamu wa mipango miji kubaini maeneo yasiyoruhusiwa kwa ajili ya makazi ya watu. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Hayo yamesemwa jana Mkuu wa Idara ya Mipango Miji, Hosiana Kusiga wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuwa wameanza kutambua maeneo yaliovamiwa, viwanja vya wazi, makaburi, masoko, shule na maeneo kwa ajili ya matumizi ya umma.

Kusiga amesema hadi sasa wameshatambua maeneo 32 yaliyovamiwa ambayo ni makaburi, masoko, shule, viwanja vya wazi, maeneo ya umma kama viwanja vya mpira wa miguu.

Aliyataja maeneo ambayo yamevamiwa na watakayoanza nayo kuyabomoa kuwa ni Nyegezi, Igoma, Nyakato, Mabatini, Mto Mirongo, Mkolani, Kishiri, Luchelele (eneo la mradi), Bugando, Bugarika (viwanja vya mpira) na shule ya sekondari Nyakurunduma.

Hata hivyo Kusiga amesema bado wanaendelea na kazi ya utambuzi katika maeneo yanayosababisha mafuriko na milima hatarishi kama Mabatini na Butimba ambayo wakati wa mvua husababisha mawe kuanguka na kudai kwamba ni lazima watu waondoke.

Aidha amesema kuwa baada ya kubaini maeneo yote watatoa taarifa kwa watu watakaokumbwa na zoezi hilo, ili waondoke wenyewe kama ni nyumba yake aweze kuivunja katika utaratibu utakaomsaidia kupata baadhi ya vifaa alivyotumia kwenye ujenzi kabla ya kuvunjiwa na Serikali.

Pia aliwataka wananchi kufikiria wataenda wapi kwani baada ya kutambua maeneo yote wataingia katika vikao vya kamati ya mipango miji ili kuwaelimisha madiwani nao wafahamu jinsi zoezi hilo litakavyo tekelezwa kwa waliovamia maeneo ya wazi na kando mwa mito.

“Wahusika watapewa taarifa ya kuondoka maeneo hayo, nilazima watu wafuate sheria kwani kujenga  mjini bila ya kibali ni kosa, zoezi hili totalisimamia kwa kufuata sheria,” amesema Kusiga.

Amesema wale wanaojenga bila mpangilio ni wale wanaouziwa vipande vya ardhi, wanaamua kujenga bila ya kufuata utaratibu na kwamba ni muhimu mtu wanapouziwa wafuate taratibu zitakazoweza kuruhusu ujenzi eneo hilo.

error: Content is protected !!