January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bomoabomoa bila vibali Mkwajuni

Spread the love

WAFANYAKAZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam leo wamebomoa makazi ya wananchi wanaoishi sehemu ya juu ya Bonde la Mkwajuni, Mtaa wa Idrisa, Kata ya Magomeni, jijini Dar es Salaam. Anaandika Regina Mkonde.

Operesheni hiyo iliyoanza majira ya saa 2 asubuhi, ilihusu nyumba tano ikiwemo ya Makamba MwinyiKondo, ambayo ndipo ilipo Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Idrisa.

Kulizuka shutuma kali dhidi ya uongozi wa Manispaa kwa kuwa operesheni ilifanywa bila ya kuwepo amri yoyote ya mahakama na wafanyakazi hawakuwa na vibali.

Akizungumza na mwandishi wa MwanaHALISI Online leo wakati ubomoaji ukiendelea, Issa Sekatawa ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Idrisa amesema waliobomoa nyumba hizo hawakufuata utaratibu unaotakiwa.

“Tunajua waliokuja kubomoa ni wafanyakazi wa Halmashauri, lakini walitakiwa kufuata taratibu zinazostahili na si kufanya kiholela, kwanza hawakuripoti rasmi kwa uongozi wa mtaa na hawakujisajili kwenye kitabu cha wageni,” amesema Sekatawa.

“Ilitakiwa waoneshe vibali ili kutuhakikishia kuwa wanahaki ya kubomoa, walivyokataa kutuonesha vibali inamaana wana nia ya kukana hapo baadae kama itajulikana kuwa wamebomoa kimakosa.”

Sekatawa amesema kuwa walipowahoji juu ya uhalali wao kwa kuonesha vibali na kusaini katika daftari la usajili, walijibiwa kuwa, kama wanataka vibali wakamuulize Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni.

Mwinyikondo amelalamika kuwa Halmashauri haikuwatendea haki kubomoa nyumba bila ya kujiridhisha kama ilikuwa ni lazima kwa kuwa hawako ndani ya bonde la Mkwajuni.

“Nyumba yangu imejengwa na Shirika la Nyumba (NHC) miaka mingi iliyopita, ramani niliyonayo haioneshi kama ilistahili kubomolewa, ila ramani mpya ndiyo inaonesha kama ninastahili kubomolewa,” amesema Mwinyikondo.

Mwinyikondo amesema hiyo ni mara ya pili nyumba yake kukumbwa na balaa la kubomolewa, mara ya kwanza ikiwa pia hakulipwa chochote.

“Nyumba yangu ndiyo kazi yangu, nimezeeka, sina uwezo wa kufanya kazi, wamebomoa sehemu ambayo ilikuwa vyumba vya wapangaji, je,wapangaji wangu nitawalipa nini na mimi nitaishi vipi, je halmashauri itanilipa au kunipa ela ya kula?”

MwanaHalisi Online ilimtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ili kujibu tuhuma hizo, lakini hakupatikana.

Hadi sasa, watu 100 kati ya waliobomolewa nyumba maeneo ya bonde la Mkwajuni, hawana makazi ya kudumu na fedha za kujikimu mahitaji yao ya kila siku imekuwa shida, kiasi cha baadhi yao kulazimika kuuza baadhi ya vitu vyao ili kupata riziki.

Sabas Gidion ambaye ni Mjumbe wa Mtaa wa Idrisa, amesema baadhi ya watu hushirikiana chumba kimoja wakiwa watano huku wengine wakiishi maisha ya kurandaranda.

“Waliobomolewa nyumba zao wanapata taabu hasa wasio na uwezo, wengine wamehifadhiwa na ndugu pamoja na jamaa, wengine wakiishi chumba kimoja zaidi ya watu wanne,” amesema Gidion.

Inasemekana nyumba zilizobomolewa zilijengwa maeneo yasiyo rasmi, na kwamba Halmashauri imetoa agizo la kuzibomoa ili upatikane mtaa utakaotumika kama barabara.

 

error: Content is protected !!