August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bomoa bomoa yaacha kilio ‘kwa Mnyika’

Spread the love

ZOEZI la kubomoa nyumba zaidi ya 100 za mtaa ya Mbezi Centre kata ya Mbezi na mtaa wa Msigani kata ya Msigani, Jimbo la Kibamba katika wilaya ya Ubungo limeacha vilio kwa mamia ya wananchi, wakiwemo wamiliki wa nyumba, wapangaji na wafanyabiashara, anaandika Pendo Omary.

Ubomoaji huo uliosimamiwa na Jeshi la Polisi umefanyika juzi na jana huku ukidaiwa kukiuka amri ya mahakama iliyoweka zuio la ubomoaji kupitia kesi Na. 716 ya mwaka huu, iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.

Katika zoezi lililofanyika jana baadhi ya wakazi wa maeneo hayo walifanikiwa kuokoa mali zao huku wengine wakiambulia patupu baada ya kushitukia tayari gari ya ubomoaji maarufu kama ‘kijiko’ imefika katika makazi yao na hivyo kulazimika kuondoka ili kunusuru uhai wao.

Kabla ya bomoa bomoa hiyo, tarehe 18 Agosti mwaka huu Wakala wa Barabara (TANROADS) walitoa notisi ya kuwataka wakazi wa maeneo hayo kubomoa kuta/majengo yaliyo ndani ya hifadhi ya barabara ili kupisha ujenzi wa barabara ya Goba-Mbezi.

Notisi hiyo iliyosainiwa na Ndyamukama, J. ambaye ni meneja wa TANROADS Jijini Dar es Salaam ilisema, “Nyumba yako/Ukuta/shimo la maji taka/uzio/fremu za biashara vimo ndani ya hifadhi ya barabara ya Morogoro kinyume cha Sheria za Barabara ikiwemo The Highway Ordinance Cap.167 kifungu Na. 52 ya mwaka 1932, The Highway Act ya mwaka 1967, Ilani ya serikali Na. 161 (G.N), Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007 na kanuni za hifadhi za barabara za mwaka 2009 kifungu (2) (d) hivyo unaombwa kubomoa.

Lakini Abasi Makuwani, katibu wa wananchi 73 waliofungua kesi katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kupinga notisi hiyo anasema kesi hiyo Na. 716 inaendelea kusikilizwa tena tarehe 7 Desemba, mwaka huu na hivyo wanashangaa kuona ubomoaji huo ukifanyika.

“Ni mgogoro wa muda mrefu kwani mwaka 2004 tulipewa notisi ya kubomoa nyumba na TANROADS lakini tarehe 4 Desemba, 2005 tukafungua kesi Na. 80/2005 kati ya Proches E. Tarimo na wenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambapo mahakama iliamua kuwa wananchi ndiyo wamiliki halali wa eneo hilo.

“Serikali iliambiwa kama inalihitaji eneo hilo kwa matumizi yoyote basi ifuate taratibu za kulipa fidia, baadaye serikali ilikata rufaa kwa kuomba muda wa nyongeza (extension of Time). Maombi yao yalikubaliwa lakini hatimaye yalifutwa kwa kukosa nia ya kuyaendesha (dismissed for want of prosecution),” amesema Makuwani.

“Nyumba yangu iliyobomolewa ina thamani ya Sh. 100 milioni. Mpaka sasa sina pa kwenda, nipo nalala na kushinda juani na familia yangu ya watu nane,” amesema Juma Mkombozi, alyekuwa mkazi wa mtaa wa Msigani.

Mkombozi anasema wakazi wa eneo hilo si wavamizi kwani seikali yenyewe ndiyo iliwahamishia hapo, mwaka 1971 kupitia mpango wa vijiji vya ujamaa na kwamba mwaka 1976 E.F.B Sengati, aliyekuwa msaidizi Msajili wa Vijiji alitoa hati Na. DSM.VC.8 ya kuthibitisha hadhi ya halmashauri ya kijiji cha Mbezi.

Humphrey Sambo, Diwani wa kata ya Mbezi amesema, “Serikali ndiyo wasimamizi wa sheria lakini wanakaidi amri ya mahakama. Jana (juzi), Humphrey Polepole, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo alisitisha zoezi la ubomoaji lakini leo (jana) limeendekea. Kuna kitu kimejificha.

Sambo amesema amelazimika kuwanunulia chakula baadhi ya wakazi waliombomolewa nyumba zao baada ya kushinda bila chakula.

Hata hivyo Polepole ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo alipofuatwa ofisini kwake hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, hali inayozua sintofahamu zaidi.

Jimbo la Kibamba linaongozwa na Mbunge John Mnyika wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huku madiwani wa kata zote sita za jimbo hilo wakiwa wanatokana na chama hicho pia.

error: Content is protected !!