August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bodi ya Mikopo yalalamikia madeni

Spread the love

BODI ya Mikopo ya Serikali za Mitaa inadai halmashauri zote nchini jumla ya Sh. 6 bilioni, anaandika Dany Tibason.

Kutokana na madai hayo, imelazimika kusitisha utoaji wa mikopo kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Taarifa hiyo ilitolewa Dodoma jana na Denis Bandija, Mkurugenzi Ofisi ya Rais Tamisemi, Kitengo cha Ukaguzi na Ufuatiliaji Fedha katika Mikoa na Halmashauri kwa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) wakati kamati hiyo ilipoihoji Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Shinyanga kwa Hesabu za Mwaka wa Fedha 2014/15.

Amesema, walilazimika kusisitisha utoaji wa mikopo kwenye halmashauri zote nchini ili waweze kuandaa mfumo sahihi wa utoaji na urejeshaji wa mikopo.

“Kuna tatizo kubwa sana katika urejeshaji wa mikopo, hivyo bodi haina pesa kabisa na ndio mana Tamisemi imesimamisha, maana kiasi hicho kinachodaiwa ni kikubwa sana na kinadhorotesha utendaji kazi wa bodi,”amesema.

Amefafanua kuwa, utaratibu huo wanaouandaa ni wa kisayansi hivyo utawezesha fedha za marejesho kuingia moja kwa moja kwenye mfuko wa bodi hiyo tofauti na ilivyokuwa awali.

Akizungunzia hatua ya kufikia uamuzi wa kusitisha mikopo hiyo amesema, uamuzi huo ulifikiwa na Tamisemi ili kuwezesha kuweka mfumo utakaosaidia halmashauri kutoa marejesho ya mikopo kwa wakati na moja kwa moja.

Amesema, mfumo uliokuwepo awali ni kwamba, halmashauri zilikuwa zinarejesha baada ya makusanyo ya fedha mbalimbali za halmashauri husika.

Hoja hiyo iliibuliwa na Issa Mangungu, Mbunge wa Mbagala (CCM) ambaye alihoji Halmashauri ya Kishapu, ni kwanini haijamaliza mradi wa ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Mhuze ambapo majibu yake yalikuwa ni kutokana na kukosa mkopo wa Sh. 150 walizotarajia kupata kutoka Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa.

Hata hivyo, mbunge huyo alionesha kutoridhishwa na uamuzi wa Tamisemi wa usitishaji wa mikopo kwa halmashauri, ambapo alitaka halmashauri ambazo ziliingia mkataba kwa ajili ya kupata mkopo, zipatiwe ili kukamilisha miradi iliyokwama.

Awali, akitoa majibu kuhusu mradi huo wa Stendi ya Mabasi Mhunze, Samson Pamphili, mhandisi wa halmashauri hiyo amesema, ujenzi huo ulikuwa wa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza imekamilika huku awali ya pili ikikamilika kwa asilimi 90 kutokana na ukosefu wa fedha.

Mhandisi huyo amebainisha kuwa, fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya mradi huo, zilikuwa Sh. 800 Milioni lakini zilizotolewa na bodi ya mikopo ni Sh. 650 Milioni hivyo kufanya uwepo wa upungufu wa Sh. 150 Milioni.

error: Content is protected !!