December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bodi ya Mikopo ya wanafunzi kuhojiwa bungeni

Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu

Spread the love

 

SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ameitaka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), ifike mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, kwa ajili ya kuhojiwa dhidi ya tuhuma za kudharau maelekezo ya Serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Spika Tulia ametoa agizo hilo leo Jumanne, tarehe 1 Novemba 2022, jijini Dodoma, baada ya shughuli za Bunge kuahirishwa kwa muda kwa ajili ya kujadili hoja iliyotolewa na Mbunge wa Biharamulo, Ezra Chiwelesa, ya kuijadili HESLB.

Bodi hiyo inatuhumiwa kushindwa kutoa ushirikiano kwa kamati iliyoundwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, kuchunguza mikopo inayotolewa kwa wanafunzi, kama inawafikia wanaostahili.

Kiongozi huyo wa Bunge, ameitaka HESLB ifike mbele ya kamati hiyo, Ijumaa ya tarehe 4 Novemba 2022, majira ya saa 7.00 mchana.

“Waziri naamini hawakusikilizi kwenye mengine, kwenye haya watakusikiliza, hawa wataitwa kwenye kamati yetu. Kwa kuwa leo Jumanne nafahamu watakuwa kwenye kipindi cha kuwasikiliza wanafunzi, siku ya Ijumaa wajikute kwenye hiyo kamati. Tutatoa fursa kamati ikishasikiliza tujue kama ni kiburi au ni kitu kingine tofauti,” amesema Spika Tulia.

Spika Tulia amesema, taarifa ya mahojiano hayo, itawasilishwa bungeni wiki ijayo kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Kuhusu tuhuma za bodi hiyo kutofuata vigezo katika utoaji mikopo, Spika Tulia amesema zitafanyiwa kazi na Bunge pindi kamati hiyo itakapowasilisha taarifa yake bungeni.

“Kwa maana ya kuichunguza kama inatoa mikopo sawa sawa, hizo sio hoja ambazo wanaitiwa mbele ya kamati, tunataka kuelezwa kama Bunge kwa nini hiyo bodi haisikilizi maelekezo. Yale mambo mengine ya hoja za vigezo tutalifanya baadae kamati itakapotuletea taarifa yake,” amesema Spika Tulia na kuongeza:

“Bunge linalokuja Januari na Februari, hilo tutalifanya wakati huo kama tutakuwa na sababu ya kuunda tume. Lakini sasa nataka kuelewa kama hicho ni kiburi au mambo mengine, kamati itatuambia vizuri.”

error: Content is protected !!