MKURUGENZI wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Serikali imeidhamini Bodi ya Mazao Mchanganyiko kupatiwa mkopo wa Sh.50 bilioni nyingine ili kwenda kununua mahindi kwa wakulima na kuyauza nje. Anaripoti Gabriel Mushi (endelea..)
Pia, amesema tayari serikali imetoa Sh.50 bilioni kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kwa ajili ya kununua mahindi mbali na Sh bilioni 14 za awali ilizopatiwa.
Msigwa ametoa kauli hiyo leo Jumapili tarehe 12 Septemba 2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na Watanzania kama ulivyoutaratibu wake wa kila wiki.
Msigwa amesema mbali na NFRA ambao wananunua mahindi kwa ajili ya usalama wa nchi, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB), ambayo inanunua mahindi kwa ajili ya biashara imepata soko la tani 100,000 nchini Kenya, tani 200,000 Sudani Kusini na tani 200,000 Shirika la Chakula duniani.
“Wakati wafanyabiashara wakinunua kilo moja ya mahindi kati ya Sh 250 hadi Sh.350 kwa kilo moja, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) itanunua Sh.500 kwa kilo ilihali Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB) itanunua kwa bei ya juu zaidi ili kumnufaisha mkulima,” amesema
“Mahindi yamezalishwa tani milioni saba wakati Tanzania matumizi yake ni tani 500,000, kwa hiyo uzalishaji ni mzuri, umekwenda mara mbili ya uzalishaji wa msimu uliopita,” amesema.
Pia, amesema bei ya mbolea imepanda kutokana na athari za Corona lakini serikali imeondoa vikwazo vyote ili kila mtu alete mbolea huku Serikali kupitia wakala wake wakihakikisha ubora.
Leave a comment